Ushirikiano wa zamani wafufuliwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ushirikiano wa zamani wafufuliwa

Kwa mujibu wa gazeti la „Washington Post“ Rais wa Marekani George W.Bush anatafuta washirika wapya baada ya viongozi wa zamani wa Uingereza na Uhispania-Tony Blair na Jose Maria Aznar kuondoka madarakani.Mwisho wa juma lililopita Bush alimkaribisha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwenye shamba lake la Crawford,Texas.Siku chache kabla,Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy alipokewa mjini Washington.

Ni wakati wa kupumua.Enzi ya mivutano kati ya pande mbili za Bahari ya Atlantik imemalizika. Anaehitaji ushahidi kuwa ukurasa mpya umefunguliwa katika uhusiano wa Marekani upande mmoja na Ujerumani na Ufaransa upande wa pili wa Atlantik,basi ushahaidi huo ulidhihirika juma lililopita.

Lakini Kansela Merkel na Rais Sarkozy walijitokeza tofauti.Kwani Rais wa Ufaransa, alipohotubia Bunge la Marekani mjini Washington aliisifu Marekani na akazungumzia uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi zao mbili kabla ya kuzuka mgogoro uliohusika na vita vya Irak,lakini hakuishughulikia mada ya Irak.Kwani anapaswa kuwa na hadhari ili asije kuitwa kijibwa kipya cha rais wa Marekani na hivyo kumrithi waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair.

Kwa upande mwingine,Kansela Merkel wa Ujerumani alikuwa mwerevu.Kwani alipokea mwaliko wa kumtembelea Rais wa Marekani kwenye shamba lake la Crawford,Texas,baada ya kuimarika kwa uhusiano wake na Bush na kuwahi kumueleza maoni yake zaidi ya mara moja.

Pande zote zinafahamu kuwa siku za Bush madarakani zinakaribia kumalizika.Kwa hivyo Merkel na Sarkozy katika siku zijazo,kisiasa watahusika na viongozi wapya.Hiyo humaanisha kuwa mkondo utakaofuatwa upangwe mapema.

Wakati huo huo rais wa Marekani akibakiwa na mwaka mmoja madarakani,anajaribu kuokoa kile kinachoweza kuokolewa.Mara kwa mara anasisitiza kuwa siasa zake hazitekelezwi kuambatana na uchunguzi wa maoni.Anasema matokeo ya sera zake yatapatikana baada ya muda mrefu.Hata hivyo Bush hataki kuondoka bila ya kuweza kuonyesha mafanikio ya aina fulani.

Marekani ni dola kuu pekee lenye uwezo na lililo tayari kujipeleka katika maeneo ya mizozo.Lakini Marekani inawahitaji washirika wenye usemi barani Ulaya.Haiwezekani tena kufanya kama vile waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld kuwaita washirika hao kama „Ulaya ya kale“.Kwani nchi zilizoitwa Ulaya „mpya“ wala hazijakaribia kuwa na usemi wa kisiasa kama vile Ujerumani na Ufaransa.

Kwa upande mwingine nchi za Ulaya pia zimetambua kuwa mizozo-kama vile hatima ya Kosovo hadi mgogoro wa Mashariki ya kati na Mabadiliko ya Hali ya Hewa duniani-haiwezi kutenzuliwa bila ya Marekani.Hata mgogoro unaohusika na mradi wa nyuklia wa Iran.Kwani anaefuata njia ya kidiplomasia atafanikiwa ikiwa atashirikiana na dola lililo tayari kutumia nguvu za kijeshi,njia zote zingine zinaposhindwa.

 • Tarehe 12.11.2007
 • Mwandishi Bergmann.C / P.Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH75
 • Tarehe 12.11.2007
 • Mwandishi Bergmann.C / P.Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH75

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com