Upinzani wa Somalia wakutana Eritrea | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Upinzani wa Somalia wakutana Eritrea

Viongozi wa upinzani wa Somalia wanaanza mkutano wa siku kumi katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, hii leo. Mkutano huo unalenga kuviungansiha vikosi vyao dhidi ya serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na Ethiopia.

Barabara ya mjini Asmara

Barabara ya mjini Asmara

Upinzani wa Somalia unaoongozwa na waislamu, unatarajiwa kufanya mkutano wake wiki moja baada ya mazungumzo ya majuma sita ya mdahalo na upatanisho, yaliyozijumulisha mbari mbalimbali za kisomali. Mkutano huo ulifanyika mjini Mogfadishu na kudhaminiwa na serikali ya mpito ya Somalia na jumuiya ya kimataifa.

Wajumbe takriban 450 wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano wa siku kumi uliopewa jina la ´Mkutano wa ukombozi wa Somalia.´ Mkutano huo unaanza leo baada ya kucheleweshwa kwa siku tano ili kuwapa muda zaidi wajumbe waweze kusafiri kwenda mjini Asmara.

Viongozi wa Somalia walio tarayi nchini Eritrea wameeleza katika mkutano wao na waandishi wa habari kwamba lengo la mkutano huo ni kuunda muungano wa upinzani kuikomboa Somalia kutokana na kukaliwa na Ethiopia na washirika wake. ´Tuna chaguo moja tu. Tunapigana na tunajilinda wenyewe pamoja na nchi yetu na tutanyakua uhuru wetu, amesema kiongozi wa ngazi ya juu wa kiislamu, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed.

Kiongozi huyo ameongeza kusema wana haki ya kuishi kwa amani na uhuru na kuyasimamia maswala yao wenyewe. Sheikh Ahmed pia amesema wataendelea kupigana mpaka watakapofikia lengo hilo.

Miongoni mwa wajumbe ni viongozi wa kiislamu, wanasiasa wa upinzani, wanazuoni, makundi ya kijamii na Wasomali wanaoishi nje ya nchi. Viongozi wanasema wanataka kuunda uongozi mwingine unaofaa na upinzani utakaoishawishi jumuiya ya kimataifa kwamba unastahili msaada kutoka kwake.

Marekani ilifanya makosa makubwa kwa kuituma Ethiopia iwe mjumbe wake nchini Somalia, amesema Jamac Mahaed Ghalib, aliyekuwa zamani waziri wa maswala ya ndani nchini Somalia na aliyewahi pia kuwa kamanda wa polisi nchini humo. Ghalib, ambaye hivi sasa ni mjumbe wa kundi moja la kijamii nchini Somalia, anahudhuria mkutano huo wa mjini Asmara. Anasema wanapinga sera za nchi za magahribi na sharti nchi hizo zielewe matatizo yanayosababishwa na hatua ya Ethiopia kuikalia Somalia kinyume cha sheria baada ya kuivamia.

Kiongozi wa mahakama za kiislamu, Shekh Hassan Aweys, anatafutwa na Marekani kwa madai ya kuwa na mafungamano na mtandao wa kundi la al Qaeda. Sehemu kubwa ya viongozi wa upinzani wa Somali wamekuwa wakiishi mjini Asmara tangu wanamgambo wa kiislamu walipofukuzwa kutoka mjini Mogadishu mapema mwaka huu na wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia waliosaidiwa na wanajeshi wa Ethiopia.

Mkutano wa mjini Asmara unafuatia mkutano uliozijumulisha mbari mbalimbali mjini Mogadishu, ambao upinzani wa Somalia nchini Eritrea uliugomea, ukitaka mkutano wa upatanisho uanze tu baada ya wanajeshi wa Ethiopia kuondoka Somalia. Kuwasili kwa majeshi ya Ethiopia nchini Somalia mwishoni mwa mwaka jana kuliusambaratisha muungano wa kiislamu na kuwatawanya viongozi wake katika nchi jirani za Afrika Mashariki na Warabuni.

Juma Ali Juma, rais wa zamani wa eneo la Puntland linalomilikiwa na Somalia, anasema mkutano wa mjini Asmara unalenga kulifikia lengo la Wasomali wote wanaopinga kukaliwa nchi yao na Ethiopia. Mkutano wa mjini Mogadishu ulivunjwa kufuatia mashambulizi kadhaa ya waasi, lakini hakuna wasiwasi mkubwa kuhusu usalama katika mkutano wa mjini Asmara.

Kuchaguliwa Eritrea kama sehemu ya kufanyia mkutano huo kumezusha wasiwasi ulimwenguni kwamba Eritrea inaitumia Somalia kama uwanja wa kupanga mashambulizi yake dhidi ya hasimu wake wa jadi, Ethiopia.

Eritrea imekanusha shutuma hizo pamoja na ripoti ya hivi majuzi iliyotolewa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliosema Eritrea inawapelekea silaha na fedha wanamgambo nchini Somalia. Vyombo vya habari vya serikali ya Eritrea vinasema Eritrea inachangia katika juhudi za kudumisha amani na uthabiti katika eneo la pembe ya Afrika.

 • Tarehe 05.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH8R
 • Tarehe 05.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH8R
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com