Umoja wa Ulaya wapongeza kufikishwa The Hague Radovan Karadzic | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 30.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Umoja wa Ulaya wapongeza kufikishwa The Hague Radovan Karadzic

Umoja wa Ulaya umepongeza kupelekwa kiongozi wa zamani wa Wasabu wa Bosnia Radovan Karadzic kwenye mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi kuzijibu tuhuma za mauaji na uhalifu wa kivita zinazomkabili.

Ndege iliyomsafirisha Radovan Karadzic ikikaribia kutua uwanja wa ndege wa mjini Rotterdam Uholanzi

Ndege iliyomsafirisha Radovan Karadzic ikikaribia kutua uwanja wa ndege wa mjini Rotterdam Uholanzi

Umoja wa Ulaya umesema umeridhishwa na kupelekwa Radovan Karadzic mjini The Hague Uholanzi ambako atakabiliana na tuhuma za mauaji ya kuangamiza jamii, uhalifu wa kivita na makosa mengine ya kukiuka haki za binaadamu. Msemaji wa tume ya Umoja wa Ulaya Amadeu Altafai, amesema kupelekwa Radovan Karadzic mjini The Hague ni hatua muhimu: “Hii ni hatua kubwa kwa sheria ya kimataifa. Hii ni hatua kubwa kwa Sabia na pia kwa ajili ya uhusiano kati ya Sabia na Umoja wa Ulaya”.

Umoja wa Ulaya umeongeza kusema kuwa nchi nyingine zote za eneo la Balkans zenye kuwa na uhusiano mzuri na nchi za magharibi ikiwemo Sabia, zitaweza kujiunga na Umoja huo wa Ulaya wakati zitakuwa tayari. Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umeitolea mwito Sabia kuendelea na juhudi za kuwatafuta hadi kuwakamata watuhumiwa wengine wawili wanaosalia mafichoni akiwemo mkuu wa majeshi ya Wasabu wakati wa vita vya Bosnia-Herzegovina mwanzoni mwa miaka ya 90, jenerali Radko Mladic. Radovan Karadzic alikamatwa wiki jana baada ya kusakwa kwa kipindi cha miaka 13. Amehamishwa katika mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi hii leo licha ya upinzani mkubwa wa vyama vya kihafidhina ambavyo jana vilifanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa Sabia Belgrade ambapo watu zaidi ya alfu 10 walishiriki.

Radovan Karadzic anatarajiwa kufikishwa kwa mara ya kwanza mbele ya majaji wa mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague hapo kesho ila kwa muda mfupi kulingana na mafisa kwenye mahakama hiyo. Jaji wa mahakama ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani ambayo ni sehemu ya mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai, atasoma mashtaka yanayomkabili Radovan Karadzic. Na mashtaka hayo ni juu ya mauaji ya kuangamiza jamii, uhalifu wa kivita na makosa mengine dhidi ya binaadamu wakati wa vita vya Bosnia-Herzegovina kati ya mwaka 1992 na 1995.

Kulingana na utaratibu wa kisheria wa mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai, mtuhumiwa anazo siku 30 ili kuyajibu mashtaka hayo kwa kupinga au kwa kuungama mbele ya mahakama juu ya makosa hayo. Watuhumiwa wengi hupenda kutoa msimamo wao pao hapo katika kikao cha kwanza cha kusomewa mashtaka.

Kulingana na mwendeshamshtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani, Radovan Karadzic anatarajiwa kusomewa mashtaka hapo kesho lakini kesi yake juu ya mauaji ya kuangamiza jamii itachukuwa miezi kadhaa kabla ya kuanza kusikilizwa. Serge Brammertz ameelezea kwamba ili kuendesha kesi juu ya makosa mazito kama hayo, itabidi kukusanya ushahidi wa kutosha wakiwemo watu walioshuhudia. Serge Brammertz amesema kukamatwa Radovan Karadzic tarehe 21 mwezi huu, ni jambo muhimu sana hususan kwa wahanga ambao walisubiri muda mrefu kabla ya siku hiyo kufika. Mwendeshamashtaka huyo wa mahakama ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani, hakusema hata hivyo ikiwa kufikishwa mahakamani Radovan Karadzic kutapelekea kuongeza muda wa mahakama hiyo ambao unamalizika mwaka 2010.

 • Tarehe 30.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EnRv
 • Tarehe 30.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EnRv
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com