Umoja wa Ulaya wamuwekea vikwazo vipya Lukaschenko | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.10.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya wamuwekea vikwazo vipya Lukaschenko

Umoja wa Ulaya umetangaza kuongeza vikwazo vyake dhidi ya utawala wa Alexander Lukaschenko wa Belarus, kupitia mkutano wa mawaziri wake wa mambo ya nje unaofanyika nchini Luxembourg.

Rais wa Belarus, Alexander Lukaschenko

Rais wa Belarus, Alexander Lukaschenko

Umoja wa Ulaya unataka kuipa serikali ya Belarus fursa ya kubadilika na hivyo imevitanua zaidi vikwazo vyake dhidi ya serikali hiyo. Tangu uchaguzi wa raisi kufanyika hapo mwaka 2010, bado utawala ungali unawaandama wapinzani.

"Belarus ndiyo dola ya mwisho kutawaliwa kidikteta barani Ulaya. Tunadhani kwamba Rais Lukaschenko anapaswa kuelewa kuwa lazima awaachie huru wafungwa wa kisiasa. Na kama hawezi kujifunza hili kwa njia rahisi, inabidi ajifunze kwa njia ngumu. Na huko ni pamoja na kuongeza vikwazo dhidi ya Belarus." Amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Uri Rosenthal.

Mawaziri hao wamekubaliana kuongeza vikwazo hivyo kwa kuongeza watu wengine 16 katika marufuku ya kusafiri na kuwazuilia akaunti zao kwenye mataifa ya Ulaya. Jumla ya watu wa karibu na Lukaschenko waliowekewa vikwazo hivi hivi sasa, imepindukia 200, yakiwemo makampuni matatu, yanayoiunga mkono serikali.

Wakati mkutano huu ukiendelea hapo jana, suala la mashambulizi ya mwishoni mwa wiki dhidi ya Wakristo wa madhehebu ya Coptic nchini Misri, lilijitokeza na kuchukuwa nafasi kubwa. Itakumbukwa kwamba watu 25 waliuawa hapo usiku wa Jumapili, jambo ambalo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema haliwezi kuvumiliwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (kushoto) na Rais wa Belarus Alexander Lukaschenko.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (kushoto) na Rais wa Belarus Alexander Lukaschenko.

"Huu ni wakati ambao utawala wa Misri unapaswa kujuwa umuhimu wa kuwepo kwa maingiliano baina ya dini, uvumilivu na pia uhuru wa watu kutekeleza imani zao nchini Misri." Amesema Westerwelle.

Pamoja na kuzungumzia ulazima wa Wamisri kuachiwa kutekeleza imani zao kwa uhuru, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, ameutolea wito utawala wa kijeshi wa nchi hiyo kuharakisha mchakato wa kidemokrasia likiwemo suala zima la kuitisha uchaguzi.

Mawaziri mbalimbali katika mkutano huu wamerejelea msimamo wao wa kuishinikiza serikali ya Syria iwache kuwakandamiza waandamanaji. Hata hivyo, hakuna vikwazo vipya vilivyotajwa dhidi ya utawala wa Rais Bashar Al-Assad.

Lakini katika hatua isiyotegemewa, mawaziri kadhaa wa Umoja wa Ulaya wameonesha utayarifu wa Umoja huo kuanzisha mawasiliano ya moja kwa moja na Baraza la Kitaifa la Syria, ambalo linawakusanya wapinzani wanaompinga Rais Assad.

"Tunataka kuwa na mawasiliano na upinzani wa Syria, kwa sababu tunataka kusaidia vuguvugu hili la kudai uhuru na demokrasia zaidi nchini Syria, na tutafurahi kuona kuwa upinzani unaungana." Amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Allain Juppe.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Italia, Franco Frattini, ametaka jambo hilo lichukuliwe kwa tahadhari, akisema kwamba ni lazima kwanza wapinzani hao wajulikane ni nani, wana mkakati gani na wana mipango ipi ya kutekeleza mkakati wao.

Suala la Libya nalo pia limepewa nafasi, ingawa kutokana na ukweli kwamba sasa Baraza la Mpito linashikilia sehemu kubwa ya nchi hiyo, na kwamba tayari aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi hayupo tena madarakani, mawaziri hawa wa mambo ya nje wameelekeza macho yao zaidi kwa Rais Assad wa Syria.

Mwandishi: Christoph Hasselbach/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza