Umoja wa Ulaya waiwekea Syria vikwazo | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya waiwekea Syria vikwazo

Umoja wa Ulaya umemuonya rais wa Syria, Bashar al Assad kumaliza ukandamizaji dhidi ya raia au akabiliwe na hatua za kumuadhibu huku umoja huo ukiridhia vikwazo dhidi ya serikali ya nchi hiyo vinavyoanza kutekelzwa leo.

default

Catherine Ashton, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton amesema vikwazo dhidi ya Syria vinajumuisha vikwazo vya silaha, marufuku ya viza za kusafiria na kuzuiliwa mali ya maafisa wanaoonekana kubeba dhamana ya kukandamizwa waandamanaji. Katika taarifa yake Bi Ashton amesema hatua ya serikali ya Syria inaenda kinyume na kanuni za kuheshimu haki za binadamu na uhuru msingi. Vikwazo hivyo vinanuiwa kuushinikiza utawala wa Syria ubadili mara moja sera yake, umalize machafuko na kuanzisha haraka mageuzi ya maana ya kisiasa.

Onyo la Bi Ashton linafuatia hatua ya Umoja wa Ulaya kuridhia rasmi hapo jana vikwazo dhidi ya maafisa 13 wa Syria wanaoonekana kuhusika na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji uliosababisha umwagikaji wa damu. Umoja huo uliidhinisha sheria na uamuzi unaoruhusu kikwazo dhidi ya bidhaa zinazouziwa Syria na nchi za kigeni, zikiwemo bidhaa za kilimo na vifaa vinavyoweza kutumika kuwatesa raia, pamoja na marufuku ya viza na kuzuiwa kwa mali. Majina ya maafisa waliolengwa na vikwazo hivyo hayakutolewa, lakini mwanadiplomasia mmoja wa Umoja wa Ulaya ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba maafisa wa serikali na wa idara ya ujasusi wamo katika orodha hiyo, pamoja na jamaa wawili wa rais Assad.

Syrien Präsident Bashar Assad in Damaskus

Rais wa Syria, Bashar Assad

Nchini Syria vikosi vya usalama jana viliwatia mbaroni maelfu ya watu kwenye oparesheni ya nyumba kwa nyumba kwa lengo la kulizima vuguvugu la maandamano dhidi ya serikali katika mji wa pwani wa Banias. Kwa upande mwingine wanaharakati wa mageuzi wanasema risasi zilirindima katika kitongoji kimoja cha mji mkuu, Damascus kilichozingirwa na wanajeshi.

Wazuiliwa kwenda Daraa

Maafisa wa Syria wameizuia timu ya wafanyakazi wa kutoa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kuutembelea mji wa Daraa ambako mamia ya watu inaripotiwa wameuwawa kwenye oparesheni ya serikali. Msemaji wa shirika la umoja huo linalotoa misaada ya kiutu, Bi Valerie Amos, amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa walitarajia kwenda Daraa jana lakini ziara yao ikaahirishwa na serikali na sasa anajaribu kutafuta maelezo kwa nini. Bi Amos amesema huenda timu hiyo ikaruhusiwa kuingia katika mji huo wiki ijayo.

Mataifa ya magharibi yameanzisha juhudi mpya ya kulishawishi baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuilaani Syria kwa kuwakandamiza waandamanaji wa upinzani. Hatua ya Syria kuizuia timu ya Umoja wa Mataifa kuingia Daraa imewasilishwa kwenye kikao cha baraza la usalama na Uingereza hapo jana.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Hamidou Oummilkhheir

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com