Umoja wa Mataifa waitaka Kirgistan ikomeshe machafuko | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.06.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa waitaka Kirgistan ikomeshe machafuko

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, Miroslav Jenca, amesema idadi ya wakimbizi wanaoyakimbia machafuko ya kikabila kusini mwa Kirgistan katika kipindi cha miaka 20 huenda ikafikia laki moja

default

Wauzbeki waliokimbia machafuko kusini mwa Kyrgistan

Hali inaelezwa kuwa tulivu nchini Kirgistan kufuatia machafuko ya umwagaji damu kati ya Wakirgiz na Wauzbeki, ambapo watu takriban 170 waliuwawa.Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimeitaka serikali ya Kirgistan izuie kuenea kwa machafuko na iendelee mbele na maandalizi ya kura ya maoni kuhusu katiba na uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimeihimiza Kirgistan isiruhusu machafuko mabaya ya kikabila yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu, kuvuruga kura muhimu ya maoni kuhusu katiba mpya iliyopangwa kufanyika Juni 27 na baadaye uchaguzi wa bunge hapo mwezi Oktoba mwaka huu. Taifa hilo maskini la Asia ya Kati limekumbwa na machafuko ya umwagaji damu kati ya Wauzbeki na Wakirgiz kufuatia mapinduzi yaliyomuondoa madarakani rais Kurmanbek Bakiyev.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, Miroslav Jenca, amesema mjini Bishkek hapo jana kwamba kura ya maoni ya Juni 27 juu ya katiba mpya na uchaguzi wa bunge wa mwezi Oktoba lazima uendelee kama ilivyopangwa licha ya matatizo yaliyojitokeza.

Naibu waziri mkuu wa Kyrgistan, Almazbek Atambayev, ameonya leo kwamba machafuko huenda yakaenea hadi mji mkuu Bishkek na eneo la Chui, kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo kiongozi huyo amesema serikali imejiandaa kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza katika maeneo hayo.

Umoja wa Mataifa umeihimiza Kirgistan izuie kuenea kwa machafuko katika eneo linalopakana na Afghanistan na kukadiria idadi ya watu wanaokimbia machafuko hayo kufikia laki moja. Takriban watu 170 wameuwawa katika miji ya Osh na Jalalabad katika machafuko mabaya zaidi ya kikabili nchini Kirgistan katika kipindi cha miaka 20.

Kirgisistan Unruhen

Mwanamume akitazama gari lilichomwa moto kwenye machafuko ya mjini Osh

Serikali ya mpito ya Kirgistan imemnyoshea kidole cha lawama Maxim Bakiyev, mtoto wa kiume wa rais aliyetimuliwa madarakani, Kurmanbek Bakiyev, kwa kulipa kiasi cha dola milioni 10 kudhamini machafuko ya kusini mwa Kirgistan.

Maxim Bakiyev alikamatwa jana na maafisa wa usalama wa Uingereza wakati ndege yake ya kibinafsi ilipotua katika uwanja wa ndege wa Farnborough. Maafisa wa Kirgistan wamesema wataitaka Uingereza umrudishe Maxim Bakiyev nyumbani ili ajibu mashtaka kuhusiana na machafuko hayo na kuvunja sheria za kimataifa kuhusu ulanguzi wa fedha. Anachungzwa na serikali ya mpito ya Kirgistan kwa ufisadi wa kibiashara kuhusu mikataba ya usafirishaji mafuta kwa kambi ya kijeshi ya Marekani, ambayo ni kituo muhimu kwa operesheni za kijeshi nchini Afghanistan.

Wakati haya yakijiri, mkuu wa maswala ya siasa wa Umoja wa Mataifa, Lynn Pascoe, ametaka kutengwe mara moja eneo litakalotumiwa kusafirishia misaada ya kiutu kwa wahanga wa machafuko nchini Kirgistan. Pascoe ametoa mwito huo wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, kuhusu hali nchini Kirgistan. Wanachama wote 15 wa baraza hilo wamelaani vikali machafuko ya Kirgistan na kutaka kuwepo utulivu.

China imesema imewaondoa raia wake 200 kutoka Kirgistan mapema leo na inapanga kuwarudisha wengine 400 baadaye leo.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 15.06.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Nr2d
 • Tarehe 15.06.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Nr2d
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com