1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Zaidi ya wapiganaji 1,000 bado wamekwama Mariupol

Grace Kabogo
10 Mei 2022

Ukraine imesema zaidi ya wapiganaji 1,000 bado wamekwama katika kiwanda cha chuma cha Azovstal kwenye mji wa Mariupol.

https://p.dw.com/p/4B6JT
Ukraine | Mariupol - Zivilisten verlasssen zerstörte Gebäude
Picha: Peter Kovalev/TASS/picture alliance

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk amesema mamia ya wapiganaji hao wamejeruhiwa, wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya na wanahitaji kuondolewa mara moja. Vereshchuk ametoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuongeza shinikizo kwa Urusi ili iruhusu wote waliojeruhiwa na wengine ambao sio wapiganaji waondoke kwenye eneo hilo la kiwanda.

Meya wa mji mkuu wa Ukraine, Kiev, Vitali Klitscho amesema kwamba karibu theluthi mbili ya wakaazi wa mji huo wamerejea baada ya kuondoka kwa wingi kutokana na uvamizi wa Urusi. Akizungumza na waandishi habari, Klitscho amesema kabla ya vita, watu milioni 3.5 waliishi Kiev na sasa theluthi mbili wamerejea.

Ukraine | Annalena Baerbock in Butscha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock Picha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock ameahidi kwamba jumuia ya kimataifa itawawajibisha waliohusika na mauaji ya raia kwenye mji wa Bucha. Ahadi hiyo ameitoa leo wakati wa ziara yake kwenye mji huo ulioko kwenye viunga vya mji mkuu wa Ukraine, Kiev. Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani amesema uhalifu mkubwa umefanywa Bucha wakati wa uvamizi wa Urusi.

Eneo ambako uhalifu mkubwa umefanyika

''Hili ni eneo ambako uhalifu mkubwa usioelezeka sio tu umetokea, bali pia umeonekana. Na ndiyo maana ni muhimu sana kwa mimi kuwa hapa leo. Tunaweza kutoa mchango mdogo kwa kusaidia katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinaadamu, kama jumuia ya kimataifa, kwa kukusanya ushahidi, kwa kuhakikisha kwamba wahalifu wanawajibishwa,'' alifafanua Baerbock.

Aidha, Baerbock pia ametangaza kuwa Ujerumani itaufungua tena ubalozi wake mjini Kiev. Waziri huyo wa Ujerumani pia amesema Ukraine inapaswa kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya, ingawa hakutokuwa na njia ya mkato ya kuwa mwanachama. Akizungumza na waziri mwenzake wa Ukraine, Dmytro Kuleba, Baerbock amesisitiza kuwa Ujerumani itapunguza kununua nishati ya Urusi hadi sifuri na kwamba hilo litabakia hivyo milele.

McLean, USA | Avril Haines, Direktorin National Intelligence
Mkurugenzi wa Idara ya ujasusi ya Marekani, Avril Haines Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Naye Mkurugenzi wa Idara ya ujasusi ya taifa ya Marekani, Avril Haines amesema nchi yake inaamini kuwa Rais wa Urusi, Vladmir Putin anajiandaa kwa mzozo wa muda mrefu nchini Ukraine na kwamba ushindi wa Urusi katika eneo la Donbas huenda usivimalize vita hivyo.

Zaidi ya watu milioni 8 wakimbizi wa ndani

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu milioni nane wanakadiriwa kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine. Watu hao wameyakimbia makaazi yao na kubakia ndani ya Ukraine. Umoja huo umesema idadi hiyo ni nyongeza ya zaidi ya watu milioni 5.9 wa Ukraine walioikimbia nchi hiyo, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari, 24.

Ama kwa upande mwingine, mkuu wa ujumbe unaofuatilia haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Matilda Bogner amesema kwamba maelfu ya watu wameuawa kuliko idadi kamili iliyotolewa ya watu 3,381. Bogner amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba idadi hiyo ni zaidi kwa sababu Mariupol umekuwa mji wa maficho ambako sio rahisi kupata taarifa, hivyo imekuwa vigumu kwao kupata taarifa zilizothibitishwa kikamilifu.

(AP, AFP, Reuters)