Ukraine: Rais Volodymyr Zelensky asema diplomasia ndio njia pekee ya kuvimaliza vita | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.05.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ukraine

Ukraine: Rais Volodymyr Zelensky asema diplomasia ndio njia pekee ya kuvimaliza vita

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema diplomasia tu ndio njia inayoweza kufanikisha kuleta amani na kuvimaliza vita vya Urusi nchini mwake badala ya kutafuta ushindi wa kijeshi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema anaamini kuwa suluhisho la kidiplomasia bado linawezekana katika kuvimaliza vita nchini mwake, licha ya mazungumzo kati ya nchi yake na Urusi kukwama kabisa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky

Baada ya mapigano makali kwa zaidi ya wiki 12 sasa, vikosi vya Ukraine vimezima majaribio ya majeshi ya Urusi ya kuuteka mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na mji wa kaskazini wa Kharkiv, lakini yanakabbiliwa na shinikizo kubwa katika jimbo la mashariki la Donbas.

Urusi pia inafanya mashambulizi makubwa katika eneo la Luhansk. Luhansk ni sehemu moja wapo katika jimbo kubwa la Donbas, ambalo Urusi imetangaza kuwa sasa ndilo lengo lake kuu nchini Ukraine.

Rais wa Marekani Joe Biden

Rais wa Marekani Joe Biden

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameomba msaada zaidi wa kijeshi, Pamoja na kwamba Rais wa Marekani Joe Biden tayari amesaini msaada mwingine wa kiasi cha dola bilioni 40 kuisaidia Ukraine kukabiliana na vita nchini humo.

Zelensky pia amesisitiza kwamba nchi yake iliyoharibiwa na vita inapaswa kupewa kipaumbele cha kujiunga na kuwa mwanachama kamili wa jumuiya ya Umoja wa Ulaya, akipinga pendekezo la Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na baadhi ya viongozi wengine wa jumuiya hiyo ya Umoja wa Ulaya kwamba nchi hiyo ipewe hadhi ya maelewano ya kisiasa na jumuiya hiyo wakati ikiusubiri hatua za kujiunga na uanachama wa umoja wa Ulaya.

Zelensky ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri mkuu wa Ureno Antonio Costa anayezuru Ukraine.

Rais wa Urusi Vladimr Putin

Rais wa Urusi Vladimr Putin

Wakati huo huo Urusi imechapisha orodha ya Wamarekani 963, akiwemo rais wa nchi hiyo Joe Biden, mmiliki wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg na mcheza filamu maarufu wa Hollywood, Morgan Freeman, kwamba wamepigwa marufuku kuingia nchini Urusi. Hatua hiyo ni baada ya orodha kama hiyo kutolewa ya kuwapiga marufuku baadhi ya warusi kuingia nchini Marekani.

Mkurugenzi Mkuu wa Facebook Mark Zuckerberg

Mkurugenzi Mkuu wa Facebook Mark Zuckerberg

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi siku ya Jumamosi pia iliweka marufuku ya kusafiri kwa Wakanada 26 kujibu vikwazo vya hivi karibuni dhidi ya nchi hiyo vilivyotangazwa na mamlaka ya Kanada.

Vyanzo:AFP/AP