Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ziarani Sudan. | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ziarani Sudan.

Mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa ametekwa katika jimbo la Sudan la Darfur, wakati ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ukiwasili jimboni humo kwa ziara ya kuhamasisha juhudi za kupatikana kwa amani.

default

Baadhi ya walinda amani wa Kikosi cha UNAMID, katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Kikosi cha pamoja cha kulinda aumani cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika jimbo hilo la Darfur -UNAMID- kimesema watu waliokuwa wamebeba silaha walimkamata mfanyakazi huyo wa Umoja wa Mataifa jana jioni akiwa nyumbani kwake katika mji mkuu wa jimbo la Darfur ya kaskazini wa El Fasher.

Msemaji wa kikosi hicho cha UNAMID, Kemal Saiki amesema watu hao wenye silaha waliingia katika makaazi ya wafanyakazi wanne wa kiraia mjini humo, na kuondoka na wawili kwa kutumia gari la kikosi hicho cha UNAMID, ambapo mmoja alifanikiwa kutoroka na mwingine bado hajulikani alipo.

Amemtambulisha mtu huyo kuwa siyo raia wa Sudan, lakini hakutoa maelezo zaidi juu yake, na kwamba inaaminika kuwa ni mfanyakazi wa kwanza wa kimataifa kutekwa katika mji huo.

Matukio ya kukamatwa kwa wafanyakazi na wanajeshi wa kulinda amani na baadaye kudai kulipwa fedha  yamekuwa yakiongezeka wakati hali ya ukosefu wa usalama nayo ikizidi kuongezeka.

Katika miezi ya hivi karibuni mapigano kati ya makundi ya waasi na majeshi ya Sudan yamekuwa yakiongezeka.

Majeshi ya Sudan yalivamia waasi  karibu na mji wa El Fasher muda mfupi kabla ya ujumbe wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao unafanya ziara nchini humo kuunga mkono juhudi za kupatikana kwa amani, kuwasili katika mji huo wa Darfur.

Wajumbe hao waliomo kwenye msafara huo, akiwemo balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Suzan Rice, leo walitarajiwaa kumtembelea Gavana wa Darfur kaskazini na wakaazi katika kambi ya wakimbizi, kabla ya kuelekea Khartoum.

Lakini ujumbe huo umefahamisha pia kwamba hauna nia ya kukutana na Rais Bashir kutokana na mashtaka yanayomkabili.

Mabalozi hao na wawakilishi kutoka katika mataifa 15 yaliyoko katika baraza la usalama la umoja wa mataifa, ikiwemo wanachama wake wa kudumu, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani wako katika ziara ya siku nne nchini humo kukagua maandalizi ya zoezi la kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa nchini humo Januari 9 na pia kulitembelea jimbo hilo la Darfur.

Wakati ulipowasili nchini humo, ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa ulipokewa kwa maandamano ya mamia ya wafuasi wa Rais wa Sudan Omar al Bashir, ambaye waranti ya kumkamata imetolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na mauaji katika jimbo la Darfur.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu laki tatu wamekufa nawengine takriban milioni 3 wameyakimbia makaazi yao katika jimbo hilo la Darfur tangu mwaka 2003.

Hata hivyo seikali ya Sudan inasema watu waliouawa ni elfu 10.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, dpa)

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 08.10.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PZ9e
 • Tarehe 08.10.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PZ9e
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com