1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yataka hatua kali kuzuia wimbi la tatu la Corona

Amina Mjahid
15 Aprili 2021

Maafisa wakuu wa afya nchini Ujerumani wameonya kwamba nchi hiyo inahitaji mikakati ya haraka kudhibiti wimbi la tatu la janga la corona.

https://p.dw.com/p/3s4x3
Coronavirus - Spahn zum Impfstoff Astrazeneca
Waziri wa afya wa Ujerumani, Jens SpahnPicha: Annegret Hilse/REUTERS

Hayo yameelezwa wakati idadi ya walioambukizwa virusi hivyo walio katika vyumba vya wagonjwa mahututi ikitarajiwa kupanda maradufu mwezi huu. 

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn ameyaomba majimbo 16 yanayounda Ujerumani kuweka mikakati zaidi haraka iwezekanavyo ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona, badala ya kusubiri wakati wa dharura.

Spahn amesema kuwapa watu chanjo dhidi ya ugonjwa huo pamoja na kuwapima pekee havitoshi kudhibiti hali.

Serikali ya shirikisho la Ujerumani inajaribu kuweka masharti magumu zaidi nchini kote kulidhibiti wimbi la tatu la virusi vya corona kutokana na miito iliyotolewa na madaktari nchini humo.

Kulingana na taasisi ya kuzuwiya na kudhibiti magonjwa nchini Ujerumani ya Robert Koch hii leo watu 29,426 wamethibitishwa kuambukizwa virusi  hivyo, idadi ambayo ni kubwa zaidi ya maambukizo ya kila siku tangu mwezi Januari.

Vifo vya COVID-19 vyapindukia milioni 1 barani Ulaya

England | Coronavirus | Impstoff von AstraZeneca
Picha: Yui Mok/empics/picture alliance

Huku hayo yakiarifiwa mkuu wa  shirika la afya duniani WHO barani Ulaya  dkt. Hans Kluge, amesema  vifo vitokanavyo na virusi vya corona barani humo pekee vimepindukia milioni moja huku akisema hali bado ni mbaya mno wakati watu milioni 1.6 wakiambukizwa virusi hivyo kila wiki.

Kauli yake inanuwiwa kusisitiza kuwa ulaya ni lazima iendelee kuchukua hatua dhidi ya virusi vya corona na kuongeza kasi ya utoaji chanjo huku aina mpya ya kirusi ikiongeza maradufu idadi ya maambukizi katika mataifa mengine ya bara hilo.

Akizungumzia wasiwasi wa hivi karibuni juu ya chanjo tofauti Dr Hans Kluge amesema hatari ya kuganda kwa damu iko juu zaidi kwa watu wanaugua ugonjwa wa COVID 19 kuliko wale wale wanaopokea chanjo ya AstraZeneca.

Maeneo mengine duniani pia hali siyo shwari

Kando na hayo, Marekani Brazil na Mexico zimerekodi vifo zaidi ya milioni 1.1 kila mmoja huku juhudi za kuvidhibiti virusi hivyo zikiendelezwa. Nchini India mambo huko pia sio mazuri.

Brasilien Sao Paolo | Coronavirus | Begräbnis | Ausschnitt VARIANTE
Picha: Amanda Perobelli/REUTERS

Hii leo serikali ya taifa hilo linalopambana na uhaba wa chanjo, matibabu na kukosa vitanda vya kutosha vya wagonjwa hospitalini limetangaza watu 200,000 kuambukizwa virusi vya corona hii leo pekee

India ambayo imeachana na mikusanyiko ya hadhara mwezi huu imeshuhudia maambukizi mapya iliyofikia milioni 2 idadi ambayo inatarajiwa kuendelea kupanda na kuchukua nafasi ya Brazili kwa kuwa taifa la pili baada ya Marekani kuwa na idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi hivyo duniani.