Ujerumani yakubaliana hatua sawa kudhibiti corona | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yakubaliana hatua sawa kudhibiti corona

Nchini Ujerumani, baraza la mawaziri la serikali ya Kansela Angela Merkel limeidhinisha hatua za pamoja za kufuatwa kote nchini humo katika kulidhibiti janga la Covid-19. 

Serikali kuu ya Ujerumani mjini Berlin imesema inataka hatua za dharura za kukabiliana na ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya Corona nchi nzima. Hatua hizo zilizoidhinishwa kisheria zitalazimika kufuatwa na majimbo yote 16 ya nchi hii na kuondowa ule mfumo uliokuwepo wa kila jimbo kufuata mkondo wake. 

Soma Zaidi: Merkel: Hatua zilizoko sasa hazitoshi kudhibiti COVID-19

'' arekebisho haya yanamaanisha ni muhimu pale patakapohusika kiwango cha juu. Tunatekeleza hatua ya dharura nchi nzima ya kuweka vizuizi. Ambako visa vya maambukizi ni zaidi ya 100, kanuni za nchi nzima zitafuatwa baadae. Na huko baadae hatua hii ya dharura ya vizuizi haitokuwa tena suala la kujadiliwa bali itatekelezwa moja kwa moja.''

Mabadiliko haya ya kisheria sasa yanabidi yaidhinishwe na bunge. Kilichofanywa na baraza la mawaziri leo Jumanne ni kuipa nguvu kubwa zaidi serikali kuu kuweka za kufuatwa kudhibiti janga hilo la virusi vya Corona nchi nzima. Mabadiliko haya yanahusu kifungo cha sheria ya Ujerumani inayosimamia suala la kuwalinda wananchi yanapohusika magonjwa ya kuambukiza.

Deutschland Bundestag Fragestunde Coronavirus Angela Merkel

Bunge la Ujerumani linatarajiwa kuidhinisha mabadiliko haya ya hatua za dharura

Ikiwa mabadiliko hayo yataidhinishwa na bunge itamaanisha hatua ya dharura ya kuweka vizuizi kupambana na kuenea maambukizo ya virusi vya Corona iliyopendekezwa na serikali ya shirikisho itatekelezwa.

Maana yake ni kwamba jimbo lolote lile Ujerumani litakalokuwa na visa vingi vya maambukizo litalazimika kisheria kutekeleza hatua zitakazowekwa na serikali kuu. Serikali inayoongozwa na chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU inataka uidhinishwaji wa mabadiliko hayo ufanyike haraka.

Hata hivyo muda wa utekelezaji utaratibu huo mpya bado haujawekwa wazi.Kiongozi wa chama hicho cha CDU bungeni Ralph Brinkhaus ameviambia vyombo vya habari Ujerumani hii leo kwamba wanataka kulikamilisha suala hili wiki hii.

Kansela Angela Merkel amesema hali ni mbaya na hivyo wanapaswa kuiangalia kwa uzito. Kansela huyo amasema wimbi la tatu la virusi vya Corona limeipiga vibaya Ujerumani na kwamba mfumo wa sasa wa utaratibu na kanuni zilizoamuliwa baina ya serikali kuu na majimbo hauwezi kulimaliza wimbi hili la tatu.

Soma Zaidi: Ujerumani: Maambukizi mapya ya corona yavuka alama 100 kwa kila watu 100, 000.

Na kwa sababu hiyo,hatua hii mpya ya dharura ya kufuatwa nchi nzima inahitajika. Lakini pia amekumbusha kiongozi huyo kwamba Ujerumani inaelekea kwenye mwanga baada ya kuzama kwenye kiza kinene.