Viongozi wa Ulaya wakubaliana kuongeza kutengeneza chanjo ya COVID-19 | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Ulaya wakubaliana kuongeza kutengeneza chanjo ya COVID-19

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuongeza utengenezaji wa chanjo ya virusi vya corona barani Ulaya na wameonya kuwa wanaweza kuzuia mauzo ya chanjo hizo.

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amesema katika mkutano wao wa kilele viongozi hao pia wamekubaliana kuimarisha utoaji wa chanjo hizo kwa nchi wanachama. Michel amesema ni muhimu kwamba wanaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza utengenzaji wa chanjo, wakati ambapo wimbi la tatu la maambukizi ya COVID-19 likiongezeka barani Ulaya.

Merkel na umuhimu wa chanjo

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amewaambia waandishi habari kwamba kwa upande mmoja wanaheshimu usambazaji wa chanjo za virusi vya corona ulimwenguni, lakini pia wanataka kuwalinda watu wao kwa sababu hiyo ndiyo njia ya kupambana na janga hilo.

''Idadi ya maambukizi inaongezeka Ulaya. Tuko kwenye wimbi la tatu la maambukizi, lakini kimsingi tuko kwenye janga jipya la kirusi kutoka Uingereza. Ni wazi kwetu sote kwamba chanjo ni njia ya kukabiliana na mzozo huu ambao ndiyo ulikuwa lengo la majadiliano yetu,'' alisisitiza Merkel.

Soma zaidi: Maambukizi yaongezeka Ulaya

Siku ya Jumatano Umoja wa Ulaya uliongeza udhibiti wa mauzo ya chanjo za COVID-19 nje ya umoja huo katika juhudi za kukabiliana na uhaba wa chanjo. Nchi za Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani ziko nyuma katika utoaji wa chanjo kuliko nchi zilizoko nje ya umoja huo kama vile Uingereza, Marekani na Israel. Kwa sehemu utoaji wa chanjo taratibu umesababishwa na masuala ya ugavi.

Katika mkutano huo wa kilele uliofanyika kwa njia ya video, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amerejea kuitaka kampuni kubwa ya madawa ya AstraZeneca kuacha kuuza chanjo zilizotengenezwa kwenye nchi za Umoja wa Ulaya.

Weltspiegel 19.03.2021 | Corona | Impfstoff AstraZeneca, Europa

Chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca

Kati ya dozi milioni 300 zinazotarajiwa kusambazwa kwenye nchi za Umoja wa Ulaya ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni, AstraZeneca inakusudia kutoa dozi milioni 100 pekee.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amezungumzia kuunga mkono utaratibu wa kudhibiti mauzo ya nje uliowekwa na Halmashauri Kuu ya Ulaya. Aidha, Kansela Merkel alizungumzia kuhusu Uingereza kupokea chanjo za COVID-19 zinazotengenezwa na Umoja wa Ulaya.

Uingereza yapokea dozi milioni 10

Uingereza ambayo ilijiondoa kwenye umoja huo imepokea dozi milioni 10 za chanjo ya virusi vya corona zilizotenegenzwa Ulaya. Kwa jumla, Umoja wa Ulaya umesafirisha takriban dozi milioni 43 za COVID-19.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Joe Biden ametangaza kufanikiwa kwa lengo lake la kuwachanja watu milioni 100 kabla ya kumaliza siku 100 za kwanza madarakani. Lengo hilo limetimia wiki iliyopita katika siku yake ya 58 madarakani.

Akizungumza na waandishi habari kwa mara ya kwanza katika Ikulu ya Marekani, Biden amesema kwa sasa analenga kuwachanja watu milioni 200 kabla ya kutimiza siku 100 za mwanzo za utawala wake, ambapo zimebaki siku 42.

(AFP, Reuters, DW)