Uharamia wa Somalia kupigwa vita | Masuala ya Jamii | DW | 29.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Uharamia wa Somalia kupigwa vita

Azimo lawasilishwa Umoja wa Mataifa kupiga vita uharamia kwenye maeneo ya bahari nchini Somalia ambao umekuwa ukizidi kupamba moto.

default

Meli ya kifahari ya kitalii Le Ponant ya Ufaransa ikiwa nje ya fukwe za Somali baada ya kutekwa nyara na maharamia hivi karibuni.

Nchi nne zimewasilisha rasimu ya azimio kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Jumatatu ambalo linayahimiza mataifa yenye nguvu kubwa za shughuli za baharini kupambana na uharamia nje ya fukwe za Somalia na kuruhusu kuwakamata maharamia katika bahari ya Somalia.

Azimio hilo linakusudia kupiga vita ongezeko la utekaji nyara wa meli kwa ajili ya kupatiwa fedha za kuzigombowa kwenye bahari nje ya mwambao wa Somalia nchi ambayo haina utawala wa sheria na ambapo eneo lake hilo limekuja kuwa mojawapo ya kanda za hatari kabisa kwa usafiri wa meli duniani.

Katika tukio lililorepotiwa hivi karibuni maharamia wa Somalia waliteka nyara meli ya uvuvi ya Uhispania na mabaharia wake 16 na baadae kuwaachilia huru baada ya kulipwa fedha za kuwagombowa dola milioni 1.2.

Rasimu ya azimio hilo ambalo shirika la habari la Uingereza Reuters limeweza kupata nakala yake imezitaka nchi ambazo zinataka kutumia njia za kibiashara baharini nje ya pwani ya taifa hilo la Pembe ya Afrika kuzidisha hatua za uratibu miongoni mwao ili kuzuwiya vitendo vya uharamia na wizi wa kutumia silaha baharini.

Azimio hilo limewasilishwa rasmi katika kikao cha faragha cha Baraza la Usalama na Marekani,Uingereza na Ufaransa pamoja na Panama ambayo meli nyingi za kibiashara husafiri kwa kutumia bendera yake.

Azimio hilo litaziruhusu nchi kuingia katika bahari ya Somalia na kutumia hatua zozote zinazowezekana kutambuwa, kuzuwiya,kukinga na kukomesha vitendo vya uharamia na wizi wa matumizi ya silaha kwa kupanda kwenye meli wanazozishuku, kuzipekuwa na kuzitwaa pamoja na kuwakamata maharamia.

Sharti lililowekwa kwenye rasimu hiyo ni kwamba nchi zenye kuchukuwa hatua hizo zinapaswa kushirikiana na serikali ya mpito ya Somalia inayopigwa vita na pia kumjulisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Wanadiplomasia wamekataa kusema azimio hilo litapitishwa lini kutokana na kile walichosema kwamba linahusisha masuala magumu ya kisheria.

Balozi wa Merekani katika Umoja wa Mataifa Zalmay Kalilzad amesema uharamia nje ya pwani ya Somalia umekuwa ukizidi kupamba moto na kuwa wa kifudhuli zaidi na kwamba wakati umefika kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukuwa hatua ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuwa serikali ya Somalia haiko katika nafasi ya kulishughulikia tatizo hilo peke yake.

Serikali yenyewe binafsi ya Somalia ililiandikia Baraza la Usalama hapo mwezi wa Februari ikiomba kuchukuliwa kwa hatua kuleta usalama kwenye maeneo yake ya bahari.Shirika la Kimataifa la Shughuli za Baharini ambalo ni la Umoja wa Mataifa pia lilimwandikia Ban mara mbili hapo mwaka jana juu ya tatizo hilo.

Utekaji nyara na uharamia imekuwa biashara ya faida na takriban Wasomali wote huwatunza vizuri mateka wao kwa kutaraji kulipwa fedha za kuwagombowa.

Imeelezwa kwamba azmio hilo limepokelewa vizuri na nchi wanachama wa Baraza la Usalama na kwamba litawasilishwa kwa wataalamu kulipitia.

Rasimu ya azmio hilo linataka nchi wanachama ambazo yumkini zikahusika na kadhia hiyo kuhakikisha kwamba wanaotuhumiwa kuwa maharamia wanafunguliwa mashtaka.

Pia inamuomba Ban kurepoti katika kipindi kisichozidi miezi mitatu ya kupitishwa kwake juu ya jinsi azmio hilo litakavyoweza kutekelezwa na katika kipindi kisichozidi miezi sita juu ya iwapo itawezekana kulitanuwa kwa maeneo mengine yanayoathiriwa na uharamia.

 • Tarehe 29.04.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DqRf
 • Tarehe 29.04.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DqRf
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com