1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UDONDOZI WA MAGAZETI

Erasto Mbwana27 Machi 2006

Maoni ya Wahariri wa magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi yamejishughulisha zaidi na matokeo ya uchaguzi wa mikoa mitatu ya Ujerumani uliofanywa jana Rheinland-Palatinate, Baden-Württemberg na Saxony-Anhalt. Mada nyingine iliyohaririwa ni mradi wa Iran wa nishati ya kinuklia.

https://p.dw.com/p/CHWY

“BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG” likijishughulisha na matokeo ya uchaguzi wa mikoa mitatu ya Ujerumani uliofanywa jana Rheinland-Palatinate, Baden-Württemberg na Saxony-Anhalt limeandika:

“Umma una busara kubwa kama vile ilivyokuwa ikishukiwa kuhusu watakaokwenda kupiga kura. Ikiwa kuna suala muhimu sana katika nchi yetu wapigaji kura wengi hujitokeza kwenda kupiga kura. Lakini ikiwa uchaguzi huo hauhusiki hata kidogo na utawala wa serikali kuu, kama vile ilivyokuwa hapo jana, basi hufurahia maisha na hali ya hewa wakitegemea tathmini ya matokeo ya uchaguzi katika vyombo vya habari. Wapigaji kura wengi hushiriki katika uchaguzi mkuu kwa lengo la kutaka kubadilisha mambo. Ikiwa hawana matatizo ndivyo ambavyo wasivyokuwa na ari tena ya kupiga kura na msimamo wao hauhusiki hata kidogo na demokrasia.”

Hayo yalikuwa maoni ya “BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG.”

“OSTTHÜRINGER ZEITUNG” nalo limeandika:

“Vyama vya mrengo wa kushoto na kile cha WASG havikupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mikoa hiyo mitatu kama vile ilivyokuwa ikitarajiwa. Kampeni kali zilizofanywa na Wanasiasa wanaojua kila kitu kama vile Lafontaine, Gysi na Ernst hazikuleta tija isipokuwa katika mkoa wa Saxony-Anhalt. Chama cha PDS kimenufaika kupata ushindi wa robo ya kura zote kutokana na ukweli kuwa watu waliokwenda kupiga kura walikuwa wachache kupita kiasi. Lakini hicho ni kizungumkuti cha kimkoa katika sehemu ya mashariki peke yake kinyume na magharibi mwa Ujerumani. Hata hivyo, vyama vya mrengo wa kushoto vitaendelea kupiga kelele na kuungana zaidi vikitegemea siku nzuri za usoni.

Maoni ya “OSTTHÜRINGER ZEITUNG.”

“BERLINER ZEITUNG” likijishughulisha na mada hiyo hiyo limeandika:

“Serikali kuu ya Berlin imeidhinishwa kutokana na matokeo ya uchaguzi uliofanywa jana katika mikoa mitatu ya Ujerumani. Serikali kuu inapaswa kutambua kuwa imechaguliwa mara mbili. Vyama vikubwa vimeimarishwa na pia muungano mkubwa. Wapigaji kura wanaamini kuwa muungano mkubwa unaweza kutatua matatizo makubwa. Lakini ingawaje ni hivyo, wapigaji kura wana matarajio yao kutoka kwa serikali ya muungano wa vyama vikubwa. Ushindi huo wa moja kwa moja una maanisha kuwa imepewa dhima maalumu. Jukumu hilo mahsusi ni la kutafuta ufumbuzi wa matatizo sugu ya ndani ya nchi.”

Hayo yalikuwa maoni ya “BERLINER ZEITUNG.”

Gazeti la “FRANKFURTER ALLGEMEINE” likijishughulisha zaidi na chama cha Social Democratic (SPD) kutawala peke yake katika mkoa wa Rheinland-Pfalz limeandika:

“Chama cha SPD, kikiwa na Waziri mkuu wake Beck, kimeimarishwa zaidi kushika uongozi wa mkoa huo kuliko vile ilivyokuwa miaka 12 iliyopita. Hayo yote yametokana na ukweli kuwa Waziri Mkuu Beck anapendwa sana na Wananchi wenzake kutokana na vile anavyotekeleza sera za serikali yake. Kinyume chake, lazima vyama ndugu vya Christian Democratic (CDU) na Christian Social (CSU) vitambue kuwa upinzani dhidi ya serikali inayofanya kila kitu vizuri na makosa yake ni machache, kimsingi ni vigumu sana kuiangusha.”

Maoni ya gazeti la “FRANKFURTER ALLGEMEINE.”

“MITTELDEUTSCHEN ZEITUNG” likijishughulisha na matokeo ya mkoa wa Saxony-Anhalt limeandika:

“Waziri Mkuu wa mkoa huo Wolfgang Böhmer anaweza kuendelea kutawala. Huo ndiyo ukweli wa mambo. Chama cha CDU kimejipatia ushindi mkubwa. Sera zinazotekelezwa na Böhmer za mkono mtulivu, uwazi na za kutafakari, bila ya wasiwasi wowote ule, zimezalisha matunda mema. Wakati chama cha CDU kimesaidiwa sana na kauli mbiyu yake ya “Tuendelee hivi hivi”, mshirika wake mdogo chama cha Free Democratic (FDP) kimeangamizwa na kutumbukia shimoni. Waliberali hawakufanikiwa hata kidogo kujipatia wingi mkubwa wa keki ya muungano wao. Chama cha SPD nacho kwa vile kimepata kura chache kuliko vile ilivyotarajia inatokana na vile jinsi kilivyoendesha kampeni zake.”

Hayo yalikuwa maoni ya “MITTELDEUTSCHEN ZEITUNG.”

Gazeti la “WESTFÄLISCHE RUNDSCHAU” likijishughulisha na mradi wa Iran wa nishati ya kinuklia limeandika:

“Ikiwa kweli Viongozi wa Iran wanataka warudishwe katika hekima na busara ni lazima jamii ya kimataifa iwe na mshikamano na kuondoa hali ya kutoelewana. Jamii ya kimataifa ina jukumu la kuiambia Iran dhahiri shahiri kuwa inapaswa kuacha mradi wake wa nishati ya kinuklia. Lakini ikiwa itaendelea kushikilia msimamo wake itakuwa hakuna njia nyingine ya kufanya isipokuwa kuchukua hatua za kijeshi. Ukarasa unaweza kufunuliwa au kufungwa na Viongozi wenyewe wa Iran.”

Kwa maoni hayo ya gazeti la “WESTFÄLISCHE RUNDSCHAU” kuhusu mradi wa Iran wa nishati ya kinuklia ndiyo yote tuliyoweza kuwakusanyia kutoka magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi.