1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UDONDOZI WA MAGAZETI

Erasto Mbwana3 Aprili 2006

Maoni ya Wahariri wa magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi yamejishughulisha zaidi na kukosolewa kwa Kansela wa zamani Gerhard Schröder kuhusu wadhifa wake mpya katika Kampuni ya Gesi ya Kirussi, Gasprom; Mkutano mkuu wa nishati ulioitishwa leo na Kansela Angela Merkel na utumiaji wa nguvu katika shule za Kijerumani.

https://p.dw.com/p/CHWU

STUTTGARTER ZEITUNG” likijishughulisha na maoni mbalimbali yanayotolewa kuhusu wadhifa mpya wa Kansela wa zamani Gerhard Schröder limeandika:

“Schröder, kutokana na kubadilisha wadhifa wake haraka kutoka ukansela hadi kuhudumia kampuni ambayo iko chini ya uongozi wa Urussi, ametia dosari siasa na nchi yake. Hajaonyesha utumishi bora. Akiwa mtu wa kawaida sasa ana nufaika na biashara ya mabilioni ya fedha ambayo ameipendekeza binafsi. Kutokana na haya yote ameusababisha Umma ufikiri zaidi na hata ile ahadi ya dhamana iliyotolewa kwa kampuni hiyo, ambayo inasababisha malumbano, iko hatarini ingawaje bado haijathibitishwa kama anahusika. Lakini vibaya zaidi ni kuona kuna hisia kuwa Kansela Schröder ametumia wadhifa wake kwa kujipatia fedha zaidi.”

Hayo yalikuwa maoni ya “STUTTGARTER ZEITUNG.”

“MITTELDEUTSCHE ZEITUNG” nalo limeandika:

“Kwa mara nyingine tena Schröder. Kwa mara nyingine tena Gasprom. Kuna hisia zinazoibukia tena kuwa Kansela wa zamani baada ya kung’atuka katika siasa amehakikisha kuwa atazidi kunufaika. Ili kufikia uamuzi kuwa Schröder alikuwa na lengo la kujinufaisha lazima kuna baadhi ya maswali yanayopaswa kujibiwa. Je, alifahamu kuhusu dhamana iliyoahidiwa kampuni hiyo? Licha ya swali hilo kujibiwa kuna umuhimu wa kupata maelezo zaidi. Kuna hisia pia inayopaswa kupatiwa jibu nalo ni ile ya je, Wanasiasa baada ya kung’atuka na kupatiwa malipo manono ya uzeeni wanapaswa kufanya kazi tena?”

Maoni ya “MITTELDEUTSCHE ZEITUNG.”

Gazeti la “RHEIN-NECKER” likijishughulisha na mada hiyo hiyo limeandika:

“Bunge la Ujerumani, Bundestag, lina jukumu la kutoa maelezo ya kinaga ubaga kuhusu suala zima. Kilichoko hapa kinahusu urafiki wa watu wawili Schröder na Putin. Swali linaloulizwa ni hili: Je, ni kitu gani kinachoruhusiwa katika siasa na uadilifu? Au maslahi ya kiuchumi yawekwe mbele zaidi bila ya kujali chochote kile? Ni jambo ambalo mtu hawezi kulivumilia hata kidogo.”

Hayo yalikuwa maoni ya gazeti la “RHEIN-NECKER.”

Gazeti la “WESER-KURIER” likimtetea Kansela wa zamani limeandika:

“Wakati Schröder na Putin walipofikia mapatano ya ujenzi wa bomba la gesi alitaka kushinda uchaguzi mkuu na kuendelea kuwa Kansela. Kitu muhimu pia ni kukumbuka kuwa Rais Chirac wa Ufaransa amemshauri atie saini haraka mkataba huo na Rais Putin ili Ulaya nayo iwe na ushawishi mkubwa katika biashara ya nishati. Ikumbukwe pia kuwa ilikuwa Rais wa Urussi aliyemwomba Schröder ashike wadhifa huo na amekubali baada ya kampuni za nishati za Ujerumani kumwomba hivyo.”

Maoni ya gazeti la WESER-KURIER.”

Gazeti la “THÜRINGER ALLGEMEINE” likijishughulisha na mkutano mkuu wa nishati ulioitishwa leo na Kansela Angela Merkel mjini Berlin limeandika:

“Maoni ya kushangaza yaliyotolewa na kampuni kubwa za nishati kabla ya mkutano inaonyesha kuwa Kansela hataweza kuleta mageuzi makubwa. Kampuni zinazohusika zinahisi kuwa iwapo mageuzi makubwa yatafanywa ndivyo ambavyo zitapoteza faida kubwa. Dalili zinazoonekana hivi sasa ni kuwa mkutano huo, unaofanywa katika ofisi ya Kansela, hautachukua uamuzi wowote ule wa kihistoria isipokuwa ni wa lazima.”

Maoni ya gazeti la “THÜRINGER ALLGEMEINE.”

Gazeti la “NEUE RUHRnalo likiwa halina matumaini makubwa ya mafanikio kupatikana katika mkutano huo limeandika:

“Kinachokosekana ni mwanzo wa mjadala mpya wa Umma. Hata ikiwa majibu hayatapatikana haraka kutokana na maswali yatakayoulizwa lakini lazima kuwe na ari na nguvu mpya ya kubuni sera za dhati za nishati. Mali ghafi zinachukua jukumu gani katika siasa za nje za Ujerumani? Ujerumani kuzidi kutegemea mali ghafi za nishati kutoka Urussi ni njia inayofaa? Ni ufundi wa aina gani unaoweza kuzingatiwa ambao unaweza kusaidiwa na fedha kutoka serikalini?”

Hayo ni maswali yanayoulizwa na gazeti la “NEUE RUHR.”

“SÜDDEUTSCHE ZEITUNG” likiamini kuwa mkutano huo unaweza kutafuta mbinu mpya limeandika:

“Mkutano lazima ufikirie kwa makini masuala ya umeme na huduma za vyanzo vya jua. Kampuni kubwa kubwa zinaendelea kushikilia njia ambazo ni za zamani sana kuwa nishati lazima kwa sehemu kubwa itokane na makaa na vinu vya kinuklia. Kampuni hizo hazifikirii hata kidogo kama nishati zinazotumiwa nyumbani siyo lazima zitoke kwenye mitambo mikubwa isipokuwa pia kama nguvu za jua. Huduma kama hizo hazitaleta tija peke yake isipokuwa pia zitasababisha mashindano. Licha ya kutegemea makaa na gesi peke yake mitambo kama hiyo siku moja inaweza kutoa gesi asilia. Kwa nini watu wasione mbali?”

Hayo yalikuwa maoni ya “SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.”

Gazeti la „WESTDEUTSCHE ALLGEMEINE“ likijishughulisha na usemi wa Waziri Mkuu wa Bavaria, Edmund Stoiber, kuhusu utumiaji wa nguvu katika shule za Ujerumani limeandika:

„Mtu hawezi kulichukulia tatizo hili kwa urahisi na kwa upesi sana kusema kuwa wageni wasiotaka kujumuishwa katika jamii ya Wajerumani wafukuzwe nchini. Hataki pia kujishughulisha na mada muhimu ya wageni kujumuishwa katika jamii ya Wajerumani na anaunga mkono hoja kuwa shule zenye matatizo yanayosababishwa na Wanafunzi wasiokuwa Wajerumani zifungwe. Kufungwa kwa shule hakumaanishi kuwa tatizo limekwisha tatuliwa.“

Maoni ya gazeti la „WESTDEUTSCHE ALLGEMEINE.“

Hatimaye, gazeti la „RHEINISCHE POST“ limeandika:

„Hatuna tatizo la shule isipokuwa la kuwajumuisha Wageni katika jamii ya Kijerumani. Kama tatizo kama hilo lipo basi linasababishwa na sera za kuwatenga Wageni na kubakia kuwa Wageni.“

Kwa maoni hayo ya „RHEINISCHE POST“ ndiyo yote tuliyoweza kuwaletea kutoka magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi.