1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UDONDOZI WA MAGAZETI

Erasto Mbwana15 Novemba 2005

Maoni ya Wahariri wa magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi yamejishughulisha na kuundwa kwa serikali mpya ya mseto na majukumu ya Jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, baada ya kuuawa Mwanajeshi wake na muaji wa kujitoa mhanga nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/CHMH

“OSTSEE-ZEITUNG” likijishughulisha na kuundwa kwa serikali kuu ya mseto limeandika:

“Serikali kuu ya mseto sasa imekamilika. Vyama vya CDU, CSU na SPD vimeidhinisha kwa wingi mkubwa kuundwa kwa serikali kama hiyo wakati wa mikutano mikuu ya vyama hivyo. Nyuma ya kura nyingi zilizopigwa Berlin, Karlsruhe na Munich siyo kwamba zinaunga mkono peke yake kuwajibika kwa ajili ya dola isipokuwa pia usemi wa Mwenyekiti wa chama cha SPD anayeng’atuka Müntefering: Upinzani ni mbaya. Madaraka na kuwajibika vinazuia kufuata nadharia moja. Kwa hiyo, serikali kuu ya mseto itakuwa na uwezo wa kutatua matatizo makubwa.”

Maoni ya “OSTSEE-ZEITUNG.”

“SÜDDEUTSCHE ZEITUNG” limeandika:

“Wingi mkubwa uliopitisha mkataba wa kuundwa kwa serikali ya mseto katika mikutano mikuu mitatu ya vyama vinavyohusika ni muhimu. Lakini mkataba wenyewe hautoshelezi majukumu ya pamoja ya kisiasa. Mkataba huo una maswali mengi kuliko majibu. Maswali ambayo bado hayajajibiwa majibu yake huenda yakapatikana wakati wa uchaguzi wa kwanza kati ya mitatu wa mikoa utakaofanywa majira ya kipupwe.”

Maoni ya “SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.”

Gazeti la “NORDBAYERISCHEN KURIER” likihisi kuwa mapatano ya kuundwa serikali ya mseto ni mzigo mkubwa kwa Kansela ajaye limeandika:

“Mwaka ujao utaamua hatima ya serikali itakayoongozwa na Bibi Angela Merkel. Ikiwa mafanikio yataweza kupatikana kutokana na mbinu ya kuongezwa kodi ya mauzo mwaka 2007, bei ya mafuta ikiwa haitapanda na thamani ya Euro kubakia kama ilivyo itakuwa msaada mkubwa kwa Ujerumani. Kinyume chake, serikali ijayo itakabiliwa na matatizo makubwa. Lakini haya yote ni makisio tu. Watu wengi, ikiwa ni haki yao, wanatarajia makubwa kutoka serikali mpya.”

Hayo yalikuwa maoni ya “NORDBAYERISCHEN KURIER.”

Gazeti la “DIE WELT” likijishughulisha na hotuba ya Kansela Gerhard Schröder anayeng’atuka limeandika:

“Schröder katika hotuba yake nzuri ya kuaga amezusha changamoto mpya kuhusu nadharia za udemokrasia wa kijamaa. Changamoto hiyo inawahusu pia Wapinzani na wale wanaofuata sera za mrengo mpya wa kati. Schröder ametilia mkazo kile kinachopaswa kufanywa na Wasocial Democrat kwa kutaja mambo mawili makubwa. Ana kiona chama chake cha SPD kama chenye hekima lakini wakati huo huo ni nguvu pekee ya kisiasa inayopigania haki na huduma sawa za jamii. SPD inahisi kuwa upepo umeanza kubadilika. Mabingwa wa mageuzi wamekwisha toa maoni yao katika midahalo mbalimbali ya televisheni. Hawakupata mafanikio na tija zinazohitajiwa za kidemokrasia. SPD itaendelea kuwapigania Wanyonge. Huo ni ukweli wa mambo.”

Hayo yalikuwa maoni ya gazeti la “DIE WELT.”

Gazeti la „CELLESCHE ZEITUNG“ likijishughulisha na kuuawa kwa Mwanajeshi wa Jeshi la Ujerumani, Bundeswehr na mshambuliaji wa kujitoa mhanga nchini Afghanistan limeandika:

„Jeshi la Ujerumani limempoteza Mwanajeshi wake wa 18 nchini Afghanistan. Mwanajeshi mwingine anarudishwa nyumbani akiwa ndani ya jeneza. Wanasiasa, kwa mara nyingine tena, wanasema kile ambacho wanazungumza mara kwa mara ikiwa hawajui waseme nini. Wanajeshi wa Ujerumani wataendelea kutekeleza majukumu yao ya hatari katika nchi za nje kwa sababu hakuna mbadala. Wanasiasa wengi wanaafiki msimamo huo.“

Hayo yalikuwa maoni ya „CELLESCHE ZEITUNG.“

Gazeti la „HANNOVERSCHE ALLGEMEINE“ likipinga dhana ya kuondolewa kwa Wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan limeandika:

„Yule anayetoa mwito wa kuondolewa kwa Wanajeshi kutokana na mauaji yaliyotokea Kabul anacheza mikononi mwa Wataliban na kusababisha hasara mbili, Hindukush na hali kadhalika barani Ulaya. Mujahidin watashangilia kupita kiasi iwapo Wanajeshi wa Ujerumani watajitoa katika kikosi cha kulinda amani cha ISAF. Waafghanistan walio wengi wanahisi kuwa kuwako kwa Wanajeshi wa Kijerumani nchini mwao kunawapa matumaini makubwa. Wajerumani hawaonyeshi peke yao nguvu za kijeshi isipokuwa pia wanataka kuona kuwa amani ya kudumu inapatikana.“

Hayo yalikuwa maoni ya gazeti la „HANNOVERSCHE ALLGEMEINE.“

Gazeti la „FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND“ nalo limeandika:

„Wataliban hivi sasa wanapambana na Wanajeshi wa Marekani katika operesheni ya „Uhuru wa Kudumu“ huku Wanajeshi wa Kijerumani wakiwa na jukumu la ujenzi mpya. Marekani lakini inataka kuwaondoa Wanajeshi wake na mazungumzo yameanza yenye lengo la kuchanganisha pamoja operesheni hizi mbili za kijeshi. Serikali mpya ya Ujerumani lazima ichukue msimamo wa dhati kuhusu suala hili. Bunge la Ujerumani, Bundestag, hivi karibuni limerefusha muda wa mwaka mmoja zaidi kwa Wanajeshi hao kuendelea kukaa Afghanistan hali kadhalika na idadi yao kuongezwa. Wanajeshi hao wanagharimu Euro Millioni 320. Mkataba mpya wa serikali ya mseto hauzungumzii hata kidogo kuhusu Afghanistan. Serikali ijayo ya vyama ndugu vya CDU/CSU na SPD lazima iwe wazi zaidi kuhusu suala hili.“

Kwa maoni hayo ya „FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND“ kuhusu majukumu ya Jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, baada ya kuuawa Mwanajeshi wake na muaji wa kujitoa mhanga nchini Afghanistan ndiyo yote tuliyoweza kuwakusanyia kutoka magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi.