TEHRAN: Iran kuulinda mpango wake wa nyuklia | Habari za Ulimwengu | DW | 23.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

TEHRAN: Iran kuulinda mpango wake wa nyuklia

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, amesema leo kwamba Iran haitakiwi kuonyesha udhaifu juu ya mpango wake wa nyuklia.

Mjumbe wa Iran katika shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia, Ali Ashgar Soltanieh, ametoa mwito mazungumzo ya kidiplomasia yaanze tena kuutanzua mzozo wa nyuklia wa Iran.

´Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limetumiwa kama chombo dhidi ya Iran. Hili ni swala la kisiasa na suluhisho lake ni kurejea tena kwenye meza ya mazungumzo.´

Rais Ahmadinejad ameapa kuwa Iran itaulinda mpango huo hadi dakika ya mwisho, huku dola kuu zikijiandaa kujadili uwezekano wa kuongeza vikwazo dhidi ya Iran.

Hapo awali naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Nicholas Burns, alisema wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani wataujadili mpango wa nyuklia wa Iran mjini London Uingereza Jumatatu wiki ijayo.

Burns aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba Marekani itataka azimio jipya la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litayarishwe ili kuitenga Iran kwa kushindwa kutimiza agizo la kusitisha shughuli zake za kurutubisha uranium kwa wakati uliowekwa.

Nicholas Burns alikuwa akizungumza saa chache baada ya shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, kuwasilisha ripoti iliyosema Iran imepuuza tarehe ya mwisho ya kusitisha urutubishaji wa uranium na kuongeza shughuli katika mpango wake wa nyuklia.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com