Tanzania yajikokota haki za binaadamu | Masuala ya Jamii | DW | 13.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Tanzania yajikokota haki za binaadamu

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu, Amnesty International, limezindua ripoti yake ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaripotiwa ikikokota miguu katika utunzaji wa haki hizo.

Wanawake wa Kimaasai kaskazini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wanawake wa Kimaasai kaskazini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kinyume na taarifa za hali ya haki za binaadamu za miaka ya nyuma, safari hii visiwa vya Zanzibar havikusimama tena kama doa jeusi kwenye taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapohusika suala la haki za binaadamu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Amnesty International, kura ya maoni ya Julai mwaka jana, ambayo iliamua kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo, ilifungua ukurasa mpya wa hadithi ya haki za binaadamu, katika sehemu ambayo iliyozoea matukio ya uvunjaji wa haki hizo kila ufikapo wakati wa uchaguzi.

Pamoja na kutaja kwamba, ucheleweshwaji wa kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, kulikaribia kuirudisha Zanzibar kwenye machafuko, ripoti hiyo haikwenda mbali zaidi.

Ripoti ya Amnesty International ya mwaka 2011

Ripoti ya Amnesty International ya mwaka 2011

Ishaaq Ismail Sharif wa Kituo cha Haki za Binaadamu na Sheria cha Zanzibar, anasema kwamba ni kweli kwamba kile kinachojuilikana Zanzibar kama Maridhiano, kimebadilisha kwa kiasi kikubwa taswira ya haki za binaadamu visiwani humo, ingawa bado kuna mengi ya kufanywa, maana kuwepo kwa haki za binaadamu si kukosekana kwa virungu na risasi za vyombo vya dola tu.

Lakini ni upande wa Tanzania Bara, ndiko ambako ripoti hii ya Amnesty International inakokutaja zaidi kwamba hali si ya kuridhisha sana, ambapo kubinywa kwa uhuru wa vyombo vya habari, ukandamizaji wa kijinsia, udhalilishaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi na maafisa wa serikali kutokuchukuliwa hatua hata wanapovunja sheria, yametajwa kuwa kikwazo kikubwa.

Ripoti hiyo inataja vitisho vya mara kwa mara vya serikali dhidi ya baadhi ya vyombo vya habari kama dalili mbaya. Ikipigia mfano wa kutishiwa kufungwa kwa magazeti ya MwanaHalisi na Mwananchi, ripoti hiyo inasema kwamba, kumekuwapo na madai ya waandishi kadhaa kutishwa na maafisa wa serikali kwa sababu ya kuandika habari za kuikosoa serikali.

Amnesty International inaikosoa serikali ya Tanzania kwa kutoitisha uchunguzi juu ya matendo ya uvunjaji wa haki za binaadamu yaliyofanywa na polisi na makampuni binafsi ya ulinzi nchini humo, hapo mwezi Julai mwaka 2009, katika eneo la Loliondo, wilaya ya Ngorongoro, kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo wanawake wa jamii ya Kimaasai walibakwa, familia kutenganishwa na watu kiasi ya 3,000 kuhamishwa makaazi yao.

Onesmo Ole Ngurumwa wa Kituo cha Haki za Binaadamu na Sheria chenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, na ambaye kituo chake kimekuwa kikifuatilia mkasa huu wa Loliondo kwa karibu. Ole Ngurumwa anasema kwamba tukio la Loliondo ni miongoni tu mwa matukio mengi ambayo Serikali ya Tanzania hufumbia macho maafisa wake wanapovunja sheria na kuvunja haki za binaadamu.

Hata hivyo, suala la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, linatajwa kwamba limepungua sana katika kipindi cha mwaka mzima uliopita, huku kukitajwa majaribio nane tu ya mauaji, mawili yakihusisha ukataji wa viungo vya siri.

Lakini bado wanaharakati wa haki za jamii hii ya maalbino nchini Tanzania, wanaripotiwa kuendelea kulalamikia vitisho kutoka kwa washukiwa na polisi ikilaumiwa kuchukua hatua za taratibu sana kuchunguza kesi za udhalilishwaji unaowapata maalbino.

Kuhusu hali ya magereza nchini Tanzania, ripoti hiyo inasema kwamba taarifa zilizokusanywa na watafiti wao, zinaonesha kuwepo kwa hali mbaya katika magereza mengi nchini humo, ambapo mengi yao yanachukuwa watu kuliko uwezo wake, huku huduma za kiafya zikiwa na chini, na pia watoto kuchanganywa na wahalifu watu wazima.

Ripoti hii iliyozinduliwa kwenye makao makuu ya Amnesty International jijini London, Uingereza, inataja pia hali ya haki za binaadamu katika nchi nyingine za Afrika ya Mashariki, zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com