Suala la wakimbizi wa Kipalestina langojea ufumbuzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.04.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Suala la wakimbizi wa Kipalestina langojea ufumbuzi

Hali za maisha ya wakimbizi wa Kipalestina ni kiini cha mkutano wa kimataifa wa siku mbili katika makao makuu ya UNESCO mjini Paris.

Nahrung für Gaza.jpg Palestinian refugees carry food aid from the United Nations Relief and Works Agency residents of Rafah refugee camp, southern Gaza Strip, Thursday, April 24, 2008. The United Nations on Thursday stopped distributing food to Palestinian refugees in Gaza because its vehicles have run out of fuel following an Israeli blockade, a U.N. official said. (AP Photo)

Msaada wa chakula kutoka Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNRWA kwa ajili ya Wapalestina katika kambi ya wakimbizi ya Rafah,kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Mkutano huo umejadili vipi Umoja wa Mataifa utaweza kupunguza matatizo yanayokabiliwa na wakimbizi wa Kipalestina pamoja na njia ya kufumbua kwa haki mgogoro wa Mashariki ya Kati kuambatana na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

"Bila ya wakimbizi wa Palestina kuruhusiwa kurejea makwao,kamwe hakutokuwepo amani pamoja na Israel."Hayo alitamka aliekuwa kiongozi wa PLO marehemu Yasser Arafat.Wakati huo katika mji wa Oslo nchini Norway alikubaliana na Israel kuwa na majadiliano ya amani na kimsingi alikubali kuwepo kwa taifa la Israel na alitunzwa Zawadi ya Amani ya Nobel pamoja na viongozi wa Israel Shimon Peres na Yitzhak Rabin.

Lakini kuhusu suala la wakimbizi,Yasser Arafat hakubadili msimamo wake hadi kifo chake,kama ilivyokuwa pia kuhusu jiji la Jerusalem.Angalao eneo la mashariki ya Jerusalem liwe mji mkuu wa taifa la Palestina. Israel inapinga yote mawili.Inasema,Jerusalem ni mji mkuu wa Israel kwa milele.Kwa hivyo hakuna cha kujadili kuhusu wakimbizi wa Kiplaestina au sivyo mlingano wa umma na sura ya taifa la kiyahudi itabadilika.

Masuala hayo mawili yalipaswa kuwekwa kando kabla ya majadiliano kuweza kufanywa na Arafat na baadae pamoja na mrithi wake Mahmoud Abbas.Wakimbizi wamezoea hilo- yaani tangu mwaka 1948 suala la hatima yao huwekwa pembeni.Wakati wa vita vya kwanza vya Mashariki ya Kati muda mfupi tu baada ya kuundwa kwa taifa la Israel,kiasi ya Wapalestina 700,000 walikimbia makwao katika miaka ya 1948 hadi 1949 na walipata hifadhi katika nchi za jirani.Baadhi yao walikimbia kwa sababu ya uoga;wengi walifukuzwa na Israel na wengine waliondoka kwa matumaini ya kurejea nyumbani kwa ushindi.Ukimbizi huo unaendelea hadi hii leo.

Idadi ya wakimbizi wa Kipalestina kote duniani ni takriban milioni tano.Wameshatambua kuwa hawana nguvu ya kuikomboa nchi yao ya asili.Wakati huo huo wanazidi kughadhibika kwa sababu juhudi zote za mchakato wa amani hazikuwapatia cho chote.Israel haikuondoka kutoka Ukingo wa Magharibi wala haikuondosha vikwazo vinavyowakabili kila siku-isitoshe sasa Israel imejenga ukuta mkubwa na hivyo maisha ya Wapalestina yamezidi kuwa magumu.

Na katika Ukanda wa Gaza wanakoishi wakimbizi tangu mwaka 1948,hali ya maisha haikuwa bora baada ya Waisraeli kuondoka eneo hilo mwaka 2005.Kwani tangu chama cha Hamas chenye msimamo mkali kunyakua madaraka,eneo hilo linajikuta katika hali ya maafa makubwa.Hata huduma za mashirika ya misada ya kimataifa zimekwama.Lakini hali imezidi kuwa ngumu kwa sababu ya mapigano na vikwazo vya kimataifa dhidi ya kundi la Hamas lisilokubali kuweka chini silaha.Kila siku hali ya umma katika Gaza inazidi kuwa mbaya.Hata ikiwa amani itarejea na huduma za misaada zitaweza kuanzishwa tena bila ya vizuizi,yote hayo hupunguza dhiki lakini hayasuluhishi tatizo la wakimbizi.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com