Shirika la Amnesty International lawasilisha ripoti ya mwaka kuhusu haki za binadamu | Masuala ya Jamii | DW | 27.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Shirika la Amnesty International lawasilisha ripoti ya mwaka kuhusu haki za binadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeupongeza mwaka jana 2009 kama mwaka muhimu kuhusu haki kwenye ripoti yake iliyotolewa jana. Limeorodhesha ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi 159

default

Claudio Cordone, katibu mkuu wa Amnesty International

Kwenye ripoti ya mwaka 2010 kuhusu hali ya haki za binadamu ulimwenguni shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, lenye makao yake makuu mjini London Uingereza, limeueleza waranti wa mahakama ya ICC wa mwaka 2009 wa kukamatwa rais wa Sudan Omar al Bashir kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, kuwa tukio kubwa muhimu linalodhihirisha kwamba hata marais walio madarakani wako chini ya sheria.

Mkuu wa shirika la Amnesty International tawi la Ujerumani, Monika Lüke anasema, "Ufanisi mkubwa ni waranti wa kimataifa wa kukamatwa rais wa Sudan Omar al Bashir mwezi Machi mwaka jana uliotoa ishara kwa wote wanaowatesa na kuwatia gerezani wengine kwamba hawawezi kufanya hivyo bila kuadhibiwa. Ni mara ya kwanza kwa rais aliye madarakani kukabiliwa na waranti ya mahakama ya kimataifa."

Bi Monika Lüke ameikosoa Urusi, Sri Lanka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Ameongeza kwamba hali ya haki za binadamu imeendelea kuwa mbaya nchini Urusi chini ya utawala wa rais Dmitry Medvedev.

Amnesty International Jahresreport 2010

Monika Lüke, kiongozi wa Amnesty International tawi la Ujerumani

Shirika hilo limezitaka serikali mbalimbali kusaini mkataba unaoitambua kikamilifu mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague Uholanzi ili kuhakikisha uhalifu chini ya sheria ya kimataifa unaweza kushughulikiwa mahala popote duniani. Marekani, Urusi, China, Indonesia na Uturuki ni miongoni mwa mataifa ambayo hayajasaini mkataba huo.

Vikosi vya usalama na maafisa wa polisi barani Afrika wamelaumiwa kwa kuwaua mamia ya watu mwaka jana 2009 lakini hawakuchunguzwa kutokana na utamaduni wa kutojali kuadhibiwa wala kuchukuliwa hatua yoyote.

Ripoti imegusia mauaji ya kiholela yaliyofanywa kwenye uwanja wa michezo katika mji mkuu wa Guinea, Conakry mwezi Septemba mwaka jana ambapo zaidi ya watu 150 waliokuwa wakishiriki kwenye maandamano waliuwawa na wanawake wakabakwa hadharani. Shirika la Amnesty International linasema uhalifu dhidi ya binadamu ulifanyika na kupendekeza kesi hiyo iwasilishwe kwa mahakama ya ICC mjini The Hague.

Shirika hilo limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali nchini Nigeria, likisema mamia ya watu huuwawa kila mwaka mikononi mwa polisi. Cameroon pia imenyoshewa kidole cha lawama huku kukiwa hakuna dalili yoyote ya serikali kuanza kuchunguza mauaji ya watu takriban 100 mnamo mwaka 2008 wakati wa operesheni dhidi ya waandamanaji.

Nchini Kenya, shirika la Amnesty International linasema serikali imeshindwa kuchunguza kikamilifu ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na 2008 ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuwawa.

Ripoti pia imeitaja Madagascar ikisema hakuna uchunguzi huru ulioanzishwa kuchunguza mauaji ya watu wasiopungua 31, mnamo Februari 7 mwaka jana wakati wanajeshi wa nchi hiyo walipowafyatulia risasi waandamanaji walipokuwa wakiandamana katika ikulu ya rais mjini Antananarivo.

Huko Zimbabwe hali ya haki za binadamu iliboreka kidogo kufuatia kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa mwezi Februari mwaka jana. Hata hivyo kuteswa na kutishwa kwa watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati wa kisiasa na wafuasi wa chama cha upinzani, Movement for Democratic Change, MDC, cha waziri mkuu Morgan Tsvangirani, kuliendelea.

Rais wa Marekani Barack Obama amekosolewa kwa kushindwa kuifunga jela ya Guantanamo Bay nchini Cuba. Wafungwa 198 waliendelea kuzuiliwa katika gereza hilo kufikia mwisho wa mwaka jana licha ya ahadi ya utawala wa Obama kulifunga kufikia Januari 22 mwaka huu.

3rd international video journalism award Berlin

Jela ya Guantanamo bay nchini Cuba

Iran imekosolewa kwa kuwakandamiza, kuwatesa, kuwakamata na kuwaua waandanaji baada ya uchaguzi wa rais wa mwezi Juni mwaka jana. Maafisa wamekosolewa kwa kubana uhuru wa mtu kujieleza, kuzuia mawasiliano ya simu za mkono na mtandao wa intaneti.

Barani Asia China iliongeza shinikizo dhidi ya wapinzani wa serikali kwa kuwazuilia na kuwatesa wanaharakati wa haki za binadamu. Maelfu ya watu wamekimbia mateso na hali ngumu ya kiuchumi nchini Korea Kaskazini na Myanmar.

Katika mzozo wa Gaza na kusini mwa Israel, vikosi vya Israel na makundi ya wapiganaji wa Palestina waliua kinyume cha sheria na kuwajeruhi raia. Maelfu ya raia wanakabiliwa na mateso na ukiukaji wa haki kutokana na ongezeko la machafuko ya kundi la Taliban nchini Afghanistan na Pakistan.

Mwandishi: Ripperger, Sabine (DW Berlin)/ZPR/Josephat Charo

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 27.05.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NYFG
 • Tarehe 27.05.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NYFG
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com