Sherehe zapamba moto kabla ya Kombe la kandanda la dunia kuanza. | Michezo | DW | 10.06.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Sherehe zapamba moto kabla ya Kombe la kandanda la dunia kuanza.

Burudani kubwa ya muziki kufanyika Soweto usiku wa leo

default

Shabiki wa soka wa Afrika kusini .

Shamra shamra za fainali za kombe la kandanda la dunia zimeanza leo huko nchini Afrika kusini mwenyeji wa mashindano hayo, kabla ya kufunguliwa rasmi kesho. Itakua mara ya kwanza kombe la dunia linachezwa katika ardhi ya Afrika .

Wakati timu ya mwisho kati ya 32 katika mashindano hayo ikiwa imewasili, taifa hilo tangu jana usiku limo katika hali ya shangwe na hoi hoi, katika hali isiyowahi kuonekana tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa wazungu wachache-apartheid- na kuchaguliwa Nelson Mandela kuwa rais wa kwanza wa kidemokrasi miaka 16 iliopita.

Baada ya maelfu ya watu kumimiminika mitaani mjini Johannesburg kuishangiria timu ya taifa Bafana Bafana, leo ilikua ni zamu ya jiji la Capetown kuwa na sherehe za aina hiyo.

Miongoni mwa sherehe hizo ni pamoja na burudani ya muziki, leo usiku itakayoonyeshwa na televisheni kote duniani,wakishiriki wanamuziki maarufu kimataifa kama Shakira na Alicia Keyes, ambapo watawaburudisha mashabiki katika uwanja wa michezo wa Orlando mjini Soweto nje ya Jo´burg.

Katika ujumbe wake kwa Shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA , Mzee Mandela amesema "Kombe la dunia 2010 ni kitambulisho cha nguvu ya mchezo wa kandanda katika kuwaleta watu pamoja bila kujali lugha, rangi au ngozi, siasa au dini yao."

Kazi zote katika viwanja vya michezo vya mashindano hayo zimekamilika kama ilivyopangwa na pia miundo mbinu ikiwa ni pamoja na treni ya mwendo wa kasi, ikiwa ni ya kwanza barani Afrika.

Lakini pamoja na hayo visa vya uhalifu vinawatia hofu baadhi ya wageni. Wahanga wa kwanza ni kikundi cha waandishi na wapiga picha wa televisheni ya China walikumbwa na janga la kuibiwa na majambazi waliokuwa na silaha. Msemaji wa serikali Themba Maseko ametoa wito kuwataka sio tu wageni bali na raia kuwa waangalifu.

Kiasi ya masahabiki laki tano wakigeni wanatarajiwa kuweko Afrika kusini kujionea mashindano hayo na waandalizi wanasema miongoni mwa viongozi mashuhuri wa kigeni wanaotarajiwa ni pamoja na makamu war ais wa Afrika kusini Joe Biden , Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon na Rais Felipe Calderon wa Mexico ambaye timu ya taifa ya nchi yake ndiyo itakayofungua dimba na wenyeji Afrika kusini.

Wakati huo huo mfalme wa soka Pele amezitaja Brazil na Uhispania kuwa ndiyo timu kali kabisa, lakini pamoja na hayo anataka kuiona timu moja ya Afrika ikicheza fainali hapo Julai 11.

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman /AFP

Mpitiaji:Josephat Charo