Raia wa Swaziland wachagua wabunge wao | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Raia wa Swaziland wachagua wabunge wao

Lakini vyama vya siasa baado ni marufuku

Uchaguzi wa wabunge wa kwanza wa iana yake chini ya katiba mpya umefanyika Ijumaa nchini Swaziland. Uchaguzi huo umekuja kukiwa kunasikika miito ya kutaka kufanyika kwa mabadiliko ya kidemokrasia nchini humo.

Viti vinavyogombaniwa katika uchaguzi wa Ijumaa katika ufalme huo ni 55.

Uchaguzi wa Ijumaa ndio wa kwanza,chini ya katiba mpya ya mwaka wa 2006 ambayo kwa njia moja ililegeza kidogo makali dhidi ya shughuli za kisiasa nchini humo.Katiba hiyo japo ilikubali uhuru wa kukusanyika lakini vyama vya kisiasa baado vilipigwa marufuku. Marufuku dhidi ya vyama imedumu miaka 35 sasa.

Na wale wote wanaogombania viti 55 vya bunge wanapaswa kuwa wanajitegemea bila kuwa wanachama wa chama chochote.

Hali hiyo inapingwa na baadhi ya wapiga kura wakitaka vyama vya kisiasa kuhalalishwa.

Kumekuwa na maandamano pamoja na ghasia za hapa na pale kabla ya uchaguzi wa Ijumaa kutokana na manunguniko ya wananchi.

Alhamisi polisi wa nchi hiyo waliwatia mbaroni viongozi kadhaa wa vyama vya wafanya kazi na pia kuwazuilia wanaharakati wengine kushiriki katika maandamano yaliyokuwa kwenye mpaka wa nchi hiyo na jirani yake Afrika Kusini.Maandamano hayo yalikuwa ya kupinga hatua ya kupiga marufuku vyama vya kisiasa.

Maafisa wa serikali walisema kuwa maandamano hayo yangevuruga utaratibu wa kura za Ijumaa.

Inakadiriwa kuwa waSwazi takriban laki nne, kati ya wote millioni moja na Ushei,ndio wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi.

Mbali na viti 55 vinavyogombaniwa ,mfalme Muswati wa tatu,chini ya katiba anakubaliwa kuwateua wabunge wengine 10.

Sio tu wanachaguliwa wabunge,lakini pia Waziri Mkuu pamoja na baraza la mawaziri.

Naibu mwenyekiti wa tume inayosimamia uchaguzi ya Swaziland, Mzwandile Fakudze,amenukuliwa na vyombo vya habari,mapema Ijumaa akisema kuwa shughuli za kupiga kura zilikuwa zinaendelea bila tatizo lolote.

Ingawa Mfalme Muswati anapendwa na raia wake lakini hisia za kukerwa na maisha yake ya kibadhirifu kila mara zinajitokeza.Mapema mwezi jana kulitokea ghasia ambapo waandamanaji walishambulia maduka kwa mawe na pia kuiba maduka na pia kuichoma basi moja.

Mfalme huyo aliorodheshwa na jarida la Forbes kama mmoja wa wafalme tajiri duniani akishika nafasi ya 15.

Miongoni mwa kero zingine ni kukataa kwake kuleta mageuzi ya kidemokrasia,na kushindwa kushughulikia masuala ya kijamii mkiwemo janga la Ukimwi,ambapo inasemekana limeiathiri vibaya nchi hiyo kuliko mataifa yote barani Afrika.

 • Tarehe 19.09.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FLGr
 • Tarehe 19.09.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FLGr
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com