Obama kuhudhuria sherehe za kumbukumbu ya majeshi ya washirika kuingia vitani katika vita vikuu vya pili vya dunia. | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.06.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama kuhudhuria sherehe za kumbukumbu ya majeshi ya washirika kuingia vitani katika vita vikuu vya pili vya dunia.

Baada ya ziara ya jana katika kambi ya mateso ya Wanazi ya Buchenwald, Ujerumani, rais Obama anaungana na rais Sarkozy wa Ufaransa, katika kumbukumbu ya majeshi ya Marekani kuingia vitani.

default

Rais wa Marekani Barack Obama alipotembelea katika kanisa Frauenkirche mjini Dresden jana Ijumaa.

Baada ya ziara jana katika kambi ya mateso ya Wanazi ya Buchenwald, Ujerumani , rais Barack Obama anaungana leo na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, katika kumbukumbu maalum ya miaka 65 tangu majeshi ya washirika yalipoingia vitani katika vita vikuu vya pili vya dunia katika mwambao wa Ufaransa wa Normandy, mojawapo ya tarehe muhimu katika historia ya vita hivyo.


Kabla ya sherehe hizi za leo, watu walioshiriki katika vita vikuu vya pili vya dunia walitoa heshima zao kwa wenzao waliopoteza maisha katika makaburi karibu na sehemu yalipotua majeshi hayo ya Marekani kabla ya sherehe hizo kubwa za kumbukumbu ya miaka 65 ya uvamizi wa majeshi ya washirika.

Katika sherehe ya jana Ijumaa bendi za jeshi zilipiga nyimbo za taifa za Marekani, Ujerumani , Uingereza na Ufaransa na Ujerumani kama waalikwa wengine waliweka mashada ya maua katikati ya makaburi hayo katika eneo la La Cambe, nchini Ufaransa. Kiasi cha wanajeshi 22,000 wa Ujerumani wamezikwa hapo si mbali sana na ufukwe wa Omaha.

Baada ya sherehe hizo , watu kadha waliozuru sehemu hiyo walibaki karibu na makaburi hayo, mahali ambapo mchungaji mmoja wa kanisa Mjerumani pamoja na wanajeshi walimzika mwanajeshi mmoja wa Ujerumani aliyegunduliwa mwaka jana.

Nchini Ujerumani rais Barack Obama ameahidi kuchukua nafasi hii kuendeleza hatua za kuleta amani katika mashariki ya kati, huku akisisitiza wajibu wa kihistoria kwa Israel wakati akitembelea kambi ya Manazi ya Buchenwald.

Akiwa pamoja na mshindi wa tuzo ya Nobel na ambaye amenusurika katika mauaji ya Holocaust ya manazi Elie Wiesel pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel , Obama anakuwa rais wa kwanza wa Marekani kutembelea kambi hiyo ya mateso ya Buchenwald katikati ya Ujerumani.

Obama alisikiliza kwa makini maelezo ya kumbukumbu ya Wiesel katika kambi hiyo ya mateso na kuweka uaridi jeupe katika ubao wa kumbukumbu kwa ajili ya wahanga wapatao 56,000.

Wiesel alikombolewa kutoka kambi ya Buchenwald Aprili 1945 na wanajeshi wa Marekani ambao ni pamoja na mjomba wa Obama , Charlie Payne. Payne mwenye umri wa miaka 84 ambaye sasa hali yake ni dhaifu , ameamua kutofuatana na rais kwenda Buchenwald, lakini atajiunga na Obama katika sherehe za maadhimisho ya mwaka wa 65 tangu majeshi ya Marekani kuingia pwani ya Normandy, nchini Ufaransa leo Jumamosi.

Wakati akiwasili katika kambi hiyo, Obama alisalimiana na vijana wa kujitolea wanaofanyakazi katika kambi hiyo ya kumbukumbu ya Buchenwal. Mkurugenzi wa kituo hicho , Volkhard Knigge, aliliongoza kundi hilo lililojumuisha pia rais Obama na kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika viunga vya kambi hiyo. Rais Obama ameeleza kuhusika kwake na kambi hiyo ya Buchenwald, kwa kuwa mjomba wake alikuwa miongoni mwa wanajeshi wa Marekani ambao waliikomboa kambi hiyo, Aprili 1945.

Obama anatarajiwa leo kushiriki katika maadhimisho ya mwaka wa 65 tangu majeshi ya washirika kuingia katika vita vikuu vya pili vya duniani nchini Ufaransa.

Lakini huenda sherehe hizo zikaingiliwa na hatua ya vyama vya wafanyakazi nchini Ufaransa kukata umeme wakati Obama atakapokutana na Sarkozy kwa chakula cha mchana kesho.

Vyama vya wafanyakazi vinavyowakilisha wafanyakazi wa ugavi wa nishati, ambao wako katika wiki ya tisa sasa ya kampeni yao ya kuongezewa mishahara, vimesema kuwa vinaweza kukata umeme katika eneo la kati la mji wa Caen, ambako viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana.

Wafanyakazi hao wa huduma za umeme tayari wamekwisha kata mara kadha umeme nchini Ufaransa katika wiki zilizopita.

►◄

Mwandishi Sekione Kitojo/AFPE/DPAE • Tarehe 05.06.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I4Fi
 • Tarehe 05.06.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I4Fi
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com