Obama kuhudhuria mkutano wa Copenhagen | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama kuhudhuria mkutano wa Copenhagen

Jinsi gani kupunguza moshi unaochafua hewa ?

Rais Obama na Hu Jintao (China)

Rais Obama na Hu Jintao (China)

Taarifa kutoka Washington, zinasema kwamba, Rais Barack Obama, ameamua sasa kuhudhuria binafsi ule mkutano wa kilele wa kuzuwia uchafuzi wa hali ya hewa utakaofanyika mwezi ujao mjini Copenhagen,Denmark.Marekani inapanga huko kutangaza mpango wake wa kwanza kabisa wa kupambana na moshi unaochafua mazingira.

Uamuzi huo ,umefufua matumaini ya mkutano huo unaosubiriwa kwa hamu kuweza sasa kukamilishwa kwa ufanisi.China na Marekani , ndizo zinazoongoza katika uchafuzi wa hali ya hewa kwa moshi huo unazidisha ujoto.Ikiitikia tangozo la Washington, China, nayo imetangaza kwa mara ya kwanza kabisa kiwango maalumu inacholenga kupunguza moshi huo .

Utawala wa Rais Obama, umejitolea kupunguza moshi unaopaa hewani na kuchafua mazingira kwa kima cha 17% kutoka kiwango cha 2005 na kuifikia shabaha hiyo ifikapo 2020.Kima hiki cha 17%, ni kasoro na vile ilivyotakiwa na Umoja wa Ulaya,Japan na wanasayansi wa Umoja wa Mataifa.

"Rais Obama kwenda Copenhagen, kutatilia nguvu mazungumzo na tunatumai kutaimarisha matumaini ya mafanikio ya mkutano huo." alisema Carol Browner, msaidizi mkuu wa Obama katika maswali ya hali ya hewa.

Rais Obama atauhutubia mkutano huo wa mazingira mjini Copenhanegn hapo Desemba 9,siku moja kabla hakuelekea Oslo kupokea zawadi yake ya amani ya Nobel.Mike Forman, makamo-mshauri wa usalama wa taifa , amesema kwamba rais Obama ameamua baada ya kutambua yanafanyika maendeleo katika mazungumzo na China, india pamoja na nchi nyengine zinazoinukia kiviwanda.

Ikulu ya Marekani (White House), imearifu kuwa, Rais Obama atauchambua mpango wa muda mrefu wa nchi yake wa kupunguza moshi huo unaochafua mazingira kwa kima cha hadi 30% kutoka kima cha 2005 hadi ifikapo 2025,halafu kupunguza tena kwa kima cha 42% ifikapo 2030 na tena 83% mwaka 2050.

Carol Browner, msemaji wa rais Obama juu ya sera za mazingira amesema kwamba, kiwango cha muda wa wastani cha kupunguza gesi hizo zinazopaa hewani ni cha 17% hii ikitegemea sheria kupitishwa katika Baraza la Senate lililogawika mno na ambalo limeahirisha hadi mwakani hatua juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Viongozi wa nchi za nje na wakereketwa wa maswali ya mazingira wana kutathmini kuhudhuria kwa rais Obama mkutano wa Copenhagen kuwa kutapalilia upepo mpya katika kikao hicho cha Desemba 7-18 kinacholenga kutunga mkataba utakoachukua mahala pa ule wa Kyoto (Japan) juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na ambao jukumu lake linamalizika 2012.

Mkuu wa UM anaehusika na maswali ya hali ya hewa Yvo de Boer, amesema ikiwa mapendekezo ya Marekani ni wazi kabisa, yaweza kusaidia kufungua njia ya kukamilishwa mkutano wa Copenhagen kwa mafanikio.

Alisema pia kwamba, dola za kiviwanda zinapaswa kujitolea zaidi upande mwengine -nao ule wa kuahidi msaada wa fedha kwa nchi masikini ili nazo zipambane na uchafuzi wa hali ya hewa.China nayo imearifu leo kwamba, itapunguza moshi unaochafua hewa kwa kima cha kati ya 40 % hadi 45% hadi ifikapo 2020 kutoka kiwango cha 2005.

Mwandishi:Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Aboubakry Liongo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com