Obama ameshinda katika Mkoa wa Wisconsin,Marekani | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 20.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Obama ameshinda katika Mkoa wa Wisconsin,Marekani

Ushindi kwa Obama

Barack Obama,mtetezi wa Urais wa Marekani kwa chama cha Democratic

Barack Obama,mtetezi wa Urais wa Marekani kwa chama cha Democratic

Barack Obama yuko katika njia ya kuelekea ushindi. Mwanasiasa huyo, mwenye umri wa miaka 46, amepata ushindi wa tisa, mara hii katika Mkoa wa Wisconsin, hivyo kuliimarisha lengo lake la kutaka kumpiku mpinzani wake anayewania pia utetezi wa urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Democratic, Seneta Bibi Hilary Clinton.

Sasa mbinyo wa kisekolojia unazidi kwa Bibi Hilary Clinton ambaye ni seneta wa mkoa wa New York. Kwani pia katika Mkoa wa Hawaii Barack Obama ana hakika ya kushinda. Hilary Clinton inambidi sasa ashinde katika mchujo wa Hapo Machi 4. Na baada ya kupata ushindi mwengine katika Mkoa wa Wisconsin na Washington, Seneta John McCain sasa anaweza kutamba kwamba ana hakika ya kuwa mtetezi wa Chama cha Republican katika uchaguzi ujao wa urais.

Ushindi wa Barack Obama katika Mkoa wa Wisconsin, mkoa wenye wakaazi walio wakulima na wafugaji wa ngombe wa maziwa, sio tu ni ushindi wa tisa katika chaguzi za mchujo za chama chake cha Democratic. Lakini ushindi huo ameupata katika mkoa ambapo Hilary Clinton, hadi nusu mwaka uliopita, alikuwa akitiliwa dau na watu wengi kwamba atapata ushindi mkubwa. Huo ni mkoa ulio na wakaazi wengi weupe, na wenye mfumo wa wakaazi kama ule wa Texas. Punde hivi Barack Obama alipojua kwamba ni mshindi, alitoa hotuba:

+ Nimesikia punde hivi kwamba tumeshinda katika Mkoa wa Wisconsin...+

Watu wapatao 20,000 waliokuwa na furaha walimsikiliza Barack Obama akitangaza jambo hilo. Mambo ni wazi sasa. Ikiwa seneta huyo, mwenye asili ya Kiafrika, ameweza kushinda katika Mkoa huo unaokaliwa na watu wengi wenye rangi nyeupe, basi ni wazi kwamba ana nafasi ya kumshinda Hilary Clinton mwezi ujao katika Mkoa wa Texas. Mkoa mdogo wa Wisconsin, kwa Barack Obama, ni kama mlango uliofungua kwa yeye kuweza kushinda katika Mkoa mkubwa wa Texas. Kinyume na Hilary Clinton, Seneta Obama alipigania kusaka kila kura katika mkoa huo mdogo badala ya kuweka nguvu zake zote kusaka kura katika mkoa wa Texas wenye wajumbe wengi. Obama aliwashukuru wapiga kura, licha ya kwamba hali ya hewa ilikuwa ya baridi kali:

+Unapokwenda kupiga kura katika Wisconsin, baridi ni kali, Grade 15 chini ya sufuri nje. Kwenda katika kituo cha kupiga kura ilikuwa sio jambo la kujipumbaza, lakini hali hiyo haijawazuwia wapiga kura kufika vituoni.+

Idadi ya watu walioshiriki katika mchujo wa Wisconsin ilikuwa kubwa. Ilibidi vituo vya ziyada viwekwe, na matokeo yalikuwa wazi kabisa. Obama alimshinda Bibi Clinton kwa asilimia 15. Seneta huyo wa mkoa wa jirani wa Illinois alifaidika wazi wazi kutokana na sheria za uchaguzi za Mkoa wa Wisconsin ambapo watu wasiokuwa wa chama chochote na wale wa Chama cha Republican hutakiwa pia kuchagua mtetezi kwa ajili ya Chama cha Democratic. Mfumo huo wa uchaguzi ulimfaidia Obama. Alipata kura nyingi kutoka kwa wanachama wa Republican na wale wasioelemea chama chochote kuliko Bibi Clinton. Baada ya ushindi huo, Barack Obama alisema:

+IKiwa tushinde katika uchaguzi wa urais mwezi Novemba, basi tunahitaji kwanza kabisa msaada wenu, shauku yenu ili Marekani ibadilike mnamo miaka minne ijayo.+

Pia katika mkoa wa Hawaii, alikozaliwa Obama, uchaguzi wa mchujo utafanyika, na huko Obama ana wafuasi wengi

Na mtetezi wa Chama cha Republican, John McCain, alisonga mbele na ushindi wake, mara hii katika Wisconsin na Washington, akimpiku mpinzani wake, Mike Huckebee. Mshindi McCain alisema hivi:

+ Nitakuwa mtetezi wa urais kwa niaba ya Chama cha Republican.+

Naam. Kuwa mtetezi wa urais ni jambo moja na kuwa rais ni jambo jingine.

 • Tarehe 20.02.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DAMH
 • Tarehe 20.02.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DAMH
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com