1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yafanya mkutano wa kuadhimisha miaka 75

4 Aprili 2024

Washirika wa NATO wamekubaliana kuendelea kuisaidia Ukraine vifaa vya kijeshi ili iendeleze mapambano yake dhidi ya Urusi. Hayo yamejitokeza leo kwenye mkutano wa kuadhimisha miaka 75 ya NATO unaoendela mjini Brusells

https://p.dw.com/p/4eROf
NATO
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg akiwa katika mkutano wa jumuiya hiyo unaoendelea nchini UbelgijiPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP/picture alliance

Washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wamekubaliana kwa pamoja kutambua na kutafuta mifumo ya ulinzi wa anga katika hifadhi zao za  kijeshi na kuituma nchini Ukraine ili kuisaidia nchi hiyo katika mapambano yake dhidi ya Urusi. Hayo yamejitokeza kwenye mkutano wa kuadhimisha miaka 75 ya NATO unaoendela mjini Brusells.

Soma zaidi. Marekani yasema Ukraine itajiunga na NATO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba ambaye amehudhuria mkutano huo, amesema kwamba mataifa wanachama wa NATO yamekubali kufanya zoezi la kutafuta na kugawa mifumo ya zaida ya ulinzi wa anga na kuipatia Ukraine.

Mataifa ya Baltiki yamesema kuwa yataipatia Ukraine silaha zaidi ili kuendeleza mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Ukraine ikiwemo risasi, magari na vifurushi vingine vya kijeshi ili nchi hiyo iendeleze mapambano yake ya kujilinda zaidi.

Belgien | Sitzung NATO Ukraine Rat in Brüssel | Baerbock und Kuleba
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba akiteta jambo na Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock kwenye mkutano wa kilele wa NATOPicha: Johanna Geron/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu wa Latvia, Evika Silina amesema nchi yake itaitumia Ukraine droni za kivita zenye thamani ya dola milioni moja kwa sasa lakini mpango wa serikali yake ni kutoa droni za aina hiyo zenye thamani ya dola milioni kumi hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Blinken: Ukraine itakuwa mwanachama wa NATO

Akizungumza katika mkutano huo wa NATO wa kuadhimisha miaka 75, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameeleza kwamba huenda Ukraine ikawa miongoni mwa mataifa wanachama wa NATO huko mbeleni.

"Ukraine itakuwa mwanachama waNATO. Kusudi letu katika mkutano huu wa kilele ni kusaidia kutengeneza njia ya Ukraine ya kuwa mwanachama, huku tukisonga mbele. Tumefanya kazi nyingi juu ya hilo katika siku chache zilizopita hapa Brussels na bado ipo kazi kubwa zaidi ya kufanywa kati ya sasa na muda utakapofanyika mkutano wa kilele. Lakini tutaona, nadhani katika mkutano huo wa kilele, kutakuwa na uungwaji mkono mkubwa sana kwa Ukraine na uhusiano wake na NATO, lakini wakati huo huo hatujapoteza dira kuhusiana na mahitaji ya Ukraine ya leo, kesho na keshokutwa, ili kuweza kuisaidia kuhimili uchokozi huu wa Urusi unaoendelea''amesema Blinken.

Belgien | NATO-Generalsekretär Jens Stoltenberg und Deutschlands Außenministerin Annalena Baerbock
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wanaoshiriki mkutano wa NATO huko Brussels, UbelgijiPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Soma zaidi. Madaktari wakataa pendekezo la kusitisha mgomo Kenya

Maadhimisho hayo ya miaka 75 yamejadili kwa kiwango kikubwa namna ya kuipa Ukraine msaada zaidi wa kijeshi ingawa baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo ya NATO wana wasiwasi iwapo rais wa zamani wa Marekani Donald Trump atamshinda mpinzani wake, rais wa sasa wa Marekani Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu.

Katika kampeni zake Donald Trump alisema Marekani haitosaidia taifa lolote mwanachama wa NATO ambalo litashindwa kuongeza bajeti ya ulinzi wake binafsi kwa walau asilimia 2 ya pato jumla.