1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yamfukuza balozi wa Ethiopia

Josephat Charo
4 Aprili 2024

Somalia imemfukuza balozi wa Ethiopia mjini Mogadishu na kuzifunga balozi mbili ndogo katika eneo lenye utawala wake wa ndani la Puntland na eneo lililojitenga la Somaliland kutokana na mgogoro wa mkataba wa bandari.

https://p.dw.com/p/4eQmL
Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.Picha: Feisal Omar/REUTERS

Hayo yalisemwa siku ya Alkhamis (Aprili 4) na maafisa wawili wa Somalia, ingawa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia, Nebiyu Tedla, alisema hawakuwa na taarifa kuhusu suala hilo.

Msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed hakujibu maombi ya kutoa kauli kuhusu jambo hilo.

Ethiopia, ambayo haina mpaka wa bahari, ilisaini mkataba mnamo Januari Mosi kukodi kilomita 20 za ukanda wa pwani ya Somaliland, eneo ambalo Somalia inasema ni himaya yake.

Soma zaidi: Mapambano makali yazuka Mogadishu watu 16 wameuwawa

Jimbo hilo la kaskazini limekuwa na utawala wake wa ndani tangu 1991 na unatambuliwa na baadhi ya nchi kuwa taifa huru.

Ethiopia ilisema inataka kujenga kambi ya jeshi huko na kuahidi uwezekano wa kuitambua Somaliland kwa mabadilishano, hatua iliyoighadhabisha Somalia na kuibua hofu mkataba huo ungeliyumbisha zaidi eneo la Pembe ya Afrika.