NATO kuujadili mgogoro wa Georgia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 19.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

NATO kuujadili mgogoro wa Georgia

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa Shirika la nchi za magharibi NATO, wanatarajiwa kukutana hii leo kujadili namna ya kukabiliana na mzozo wa Georgia na mstakabali wa uhusiano baina ya Shirika lao na Urusi

Bendera za nchi wanachama mbele ya makao makuu ya Shirika la NATo mjini Brussels Ubelgiji

Bendera za nchi wanachama mbele ya makao makuu ya Shirika la NATo mjini Brussels Ubelgiji

Baada ya vita kutulia, nchi za magharibi zimeanza kutafakari juu ya mzozo wa Georgia. Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa Shirika la nchi za magharibi NATO, wanatarajiwa kukutana hii leo kwenye makao makuu ya Shirika la NATO mjini Brussels Ubelgiji, ambapo litazungumziwa pia suala la uhusiano kati ya nchi zao na Urusi mnamo siku zijazo. Nchi hizo za magharibi zinaishutumu Urusi kuwa ilitumia nguvu kupita kiasi katika mzozo wa Georgia juu ya eneo la Ossetia ya kusini, linalopigania kujitenga na Georgia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, amekiri kuwa suluhisho la mzozo wa Georgia ni gumu ila hatua ya kusitisha mapigano iliyofikiwa ni jambo linalotia moyo:

´´Katika mzozo huu, tunashukuru kuwa tumepata usitishwaji mapigano na utatupa muda mrefu wa kulishughulikia suala hilo. Suluhisho bado ni gumu kama ilivyoonekana katika hatua za kusitisha mapigano. Inaonyesha kuwa muda si mrefu tutapata makubaliano kama tulivyozielezea pande zote mbili kwamba kusitisha mapigano ni suala muhimu.´´

Kufuatia mazungumzo hayo ya Shirika la NATO, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleeza Rice, anatarajiwa kusafiri kuelekea mjini Warsaw nchini Poland ambako anatazamiwa kusaini mkataba muhimu wa ulinzi wa makombora na Poland. Hati ya mwanzo ya mkataba huo ilisainiwa hata kabla ya Georgia na Urusi kusaini mkataba wa kusitisha mapigano. Mkataba huo utairuhusu Marekani kuweka makombora ya kunasa makombora mengine kwenye ardhi ya Poland. Mpango huo ni kiini cha mzozo kati ya Marekani na Urusi. Marekani ilisema mfumo huo ni kwa ajili ya kujihami dhidi ya mashambulizi ya makombora kutoka kwa nchi ilizozitaja ''nchi za wahuni''. Urusi inauona mpango huo kama kitisho kwa usalama wake kinacholenga kuharibu mtandao wake wa kinyuklia wa kuzuwia mashambulizi.

Hapo kabla, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema mkataba huo kati ya Marekani ni Poland juu ya suala la makombora, ni kitendo ambacho hakitakwenda bila kuadhibiwa.

Na baada ya Poland, nchi ya Ukraini ilitangaza kuwa nchi ya magharibi ambayo ingependa kushirikiana nayo katika masuala ya makombora imekaribishwa. Kuna athari suala hilo la makombora likazidisha mvutano katika eneo hilo.

Mkutano huo wa Shirika la NATO, utafanyika kukiwa bado taarifa za kutatanisha juu ya majeshi ya Urusi kuondoka kutoka Georgia kama sehemu ya utekelezwaji wa mkataba wa kusitisha mapigano uliowasilishwa na Ufaransa kwa niaba ya Umoja wa Ulaya.

 • Tarehe 19.08.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F0ZJ
 • Tarehe 19.08.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F0ZJ
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com