1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

080409 Südafrika Investitionsstandort

Charo Josephat24 Aprili 2009

Kampuni ya Fahnenfleck yapeperusha bendera ya Ujerumani nchini Afrika Kusini

https://p.dw.com/p/HdXK
Mji wa Capetown nchini Afrika KusiniPicha: J. Sorges

Licha ya kuwa na kiwango cha juu cha uhalifu na kuyumba kwa sarafu yake, Afrika Kusini ni nchi ambayo inawavutia sana wawekezaji wa kampuni za Ujerumani. Wakati huu kuna kampuni 400 za Kijerumani ambazo zimejiandikisha katika shirika la biashara la kijerumani huko Afrika Kusini. Kati ya kampuni kubwa kama vile Mercedes Benz kampuni ndogo na kampuni za kati pia zimejiandikisha.

Afrika Kusini inauhitaji sana uwekezaji wa moja kwa moja kuliko nchi yeyote barani Afrika. Hata miaka 15 baada ya kumalizika rasmi kwa utawala wa ubaguzi wa rangi, pengo kati ya masikini na matajiri bado haliko karibu kuzibwa na ukosefu wa ajira kati ya wananchi weusi uko juu mno. Mgogoro wa kifedha umeikumba sana Afrika kusini, nchi ambayo ilikuwa imeingiliana vyema na masoko ya fedha ya kimataifa kuliko nchi jirani.

Jengo la kiwanda cha kisasa kilicho karibu na uwanja wa ndege wa Capetown. Wakati ambapo nje mashine nzito zinachimba na kufanya kelele, kiwanja cha ndege kinakarabatiwa kwa ajili ya mashindano ya kuwania kombe la dunia la kandanda. Ni cherehani zinazofanya kelele nyingi.

" Unaona sasa ninashona maelezo ya jinsi ya kuosha kitambaa cha bendera. Lakini ni nani anayeyahitaji maagizo haya? Kwa hakika ni wazi kuwa, kitambara hiki chenye rangi nyingi ambacho kinashonwa kwa mkono katu hakioshwi kwa mashine kwani vitambaa hivyo ni vya thamani sana mbali na ukubwa wake."

FahnenFleck ni kampuni ya kitamaduni iliyoko kaskazini mwa Ujerumani, ambayo inaendeshwa kwa sasa na kizazi cha nne. Tangu mwaka wa 1882 inazitengenezea serikali na makampuni ya kimataifa bendera na nembo zao.

Kati ya wateja wa kampuni hii watu wa heba kubwa na vile vile waliozusha utata kama vile rais wa zamani wa Liberia William Tubmann na kiongozi wa Libya, kanali Muamar Gaddafi. Nchi kama vile Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu zinaiamini kampuni ya FahnenFleck kuzitengenezea bendera zao. Pia kampuni kama vile Shell, Unilever ama McDonald zinatengenezewa nembo zao. Na wakati Umoja wa Mataifa unapopeperusha benbera yake katika mto wa Hudson huko New York nchini Marekani, bendera hiyo pia imetoka Pinneberg, Ujerumani.

Logo WM 2010 Südafrika
Nembo ya mashindano ya kombe la dunia la kandanda nchini Afrika Kusini mwaka 2010Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mara ya kwanza mashindano ya kuwania kombe la dunia la kandanda yanatarajiwa kufanyika mwaka wa 2010 katika nchi ya bara la Afrika. Hili litakuwa tukio kubwa ambalo litahitaji idadi kubwa ya bendera, nembo na mabango ya kila aina ya rangi.

Kwa mantiki hii itakuwa vyema kwa kampuni ya FahnenFleck nchini Afrika Kusini kuchukua jukumu hilo na kuwakilisha. Kwa sasa kampuni hiyo iko katika mradi wa pamoja na kampuni nyingine lakini kuanzia majira ya kiangazi mwaka huu kampuni hiyo inatarajia kufungua kiwanda chake binafsi mjini Cape Town.

Mkurugrnzi wa kampuni hiyo Bwana Jörgen Vogt anaeleza kwa nini. "Hata wateja wa Afrika kusini wametambua ubora na husema kuwa wanataka vitu thabiti na huagiza bidhaa kutoka nje kama vile Ulaya. Gharama huwa kubwa na kama mtu anaweza kutengeneza vitu hapa hapa, basi kutakuwa na manufaa kwa sababu gharama zitapungua na pia itakuwa haraka."

Mnamo Machi 16 chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini kiliagiza bendera 20,000 kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi. Bendera hizi zilihitajika siku iliyofuata jambo ambalo kampuni ya FahnenFleck haingeweza kufanya wala kuziagizia kutoka Ujerumani. Bwana Vogt anasema hii inadhihirisha umuhimu wa kutengeneza bendera hizi nchini Afrika Kusini kutokana na mahitaji ya dharura yanayoweza kutokea.

Wakati wa mashindano ya kombe la dunia la kandanda yaliyofanyika Ujerumani mwaka wa 2006, Bwana Jörgen Vogt alitafuta kampuni ambayo angeweza kushirikiana nayo nchini Afrika Kusini. Kampuni hiyo shirika ilitakiwa kuwa na uhusiano mzuri wa kiuchumi na kisiasa na pia iwe na sera ya kuwawezesha Waafrika weusi nchini humo kwa kuwapa ajira. Sera hiyo inakosolewa kuwa ubaguzi dhidi ya Wazungu.

Kampuni ya FahnenFleck ilikuwa na bahati kwani ilipata mshirika aliyekuwa na ushawishi wa kisiasa. Kutokana na hilo kampuni ya FahnenFleck imetimiza masharti yaliohitajika.

Kampuni ya Fahnenfleck ndiyo kampuni pekee yenye nafasi nzuri ya kupata kandarasi ya kutengeneza bendera, vibandiko na mabango wakati wa mashindano ya kuwania kombe la dunia la kandanda la FIFA hapo mwaka ujao nchini Afrika Kusini. Kampuni hiyo imechukua sehemu kubwa ya soko nchini Afrika Kusini, katika kutengeneza vitu vinavyotoka nchini humo vyenye vibandiko vinavyosema, "Tunajivunia kutoka Afrika Kusini".

Mwandishi: Ludger Schadomsky/Josephat Charo

Mhariri: Saumu Mwasimba