Mwanachama wa bodi ya benki kuu Sarrazin aonywa | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 03.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mwanachama wa bodi ya benki kuu Sarrazin aonywa

Mjadala wapamba moto kuhusu jinsi ya kuendelezwa na kutekelezwa juhudi za kuwajumuisha ipasavyo wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii

Thilo Sarrazin (kulia) katika mahojiano kwa njia ya televisheni kuhusu kitabu chake kinachozusha mabishano-Ujerumani yajitokomeza

Thilo Sarrazin (kulia) katika mahojiano kwa njia ya televisheni kuhusu kitabu chake kinachozusha mabishano-"Ujerumani yajitokomeza"

Thilo Sarrazin huenda akapoteza cheo chake kama mwanachama wa bodi kuu ya benki kuu ya Ujerumani kutokana na matamshi yake ambayo baadhi mtu anaweza kusema ni matusi dhidi ya wahamiaji. Wenzake katika bodi kuu ya benki kuu ya Ujerumani jana wamemuomba kwa sauti moja rais wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Christian Wulff, "amvue cheo chake.Kitabu chake alichokipa jina "Ujerumani yajitokomeza" kimechochea mjadala mkali kuhusu sera za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya jamii humu nchini.

Cheo cha Thilo Sarrazin katika benki kuu ya Ujerumani, kimsingi, ameshakipoteza. Hata kama bado rais wa shirikisho hajapitisha rasmi uamuzi wake, lakini wengi wanategemea itakua hivyo.

Idadi kubwa ya wanaompinga Sarrazin wanapumua. Lakini ushindi dhidi ya mchokozi kama huyo asiyekwisha kunung'unika una maana gani? Hauna maana kubwa, kinyume na jinsi watu wengi wanavyoamini.

Kwa sababu, kwanza mengi kati ya yale yaliyosemwa na Sarrazin kuhusu mitindo ya kutopendelea kusoma sana hasa miongoni mwa familia za wahamiaji kutoka Uturuki na nchi za Kiarabu yana ukweli ndani yake. Hata wakosoaji wake hawapingi.

Pili hakuna anaetegemea kwamba bwana huyo mjuba ataufumba mdomo wake siku za mbele. Seuze tena vituo vya televisheni na vyombo vyengine vya habari havitaacha kumfungulia jukwaa atakapokua hafanyi tena kazi ya serikali.

Waziri huyo wa zamani wa serikali ya jimbo la Berlin anastahili kulaumiwa kwa kupalilia makali ya mjadala kuhusu sera za uhamiaji. Mada tete kama hiyo kuizusha namna hiyo, si hasha ikimgeukia. Hayo ni kwa mtazamo wa wengi ambao kinyume na Sarrazin wanapendelea pawepo mjadala wa dhati tena bila ya mori.

Anaeachia yaliyomo katika kitabu chake yachapishwe na magazeti ya umma yalio ya kawaida, bila ya shaka anadhamiria zaidi kuchochea hofu na wasi wasi na kujipendekeza badala ya kusaka ufumbuzi wa tatizo lenyewe hasa.

Anaejidai kwamba Sarrazin amezungumzia mada ambayo ni miko, anakosea. Kwa miaka sasa watu wamekua wakizungumzia na kuandika pia kuhusu kasoro zilizoko katika kujumuishwa wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii humu nchini. Kuhusu shule zenye idadi kubwa ya watoto wa kigeni na ambao hawazungumzi vizuri Kijerumani. Kuhusu mitaa ambayo polisi wanaiepuka kwasababu hawajisikii salama kutokana na idadi kubwa ya wageni wanaoishi. Kuhusu vijana wanaotumia nguvu na wauza madawa ya kulevya. Hakuna kinachofichwa.

Kinachokosekana ni hatua thabiti za kupambana na hali hiyo.Lawama hizo wanasiasa wamekuwa wakitupiwa tangu miaka kadhaa sasa. Ni nadra kuona matamshi yao yanatekelezwa kivitendo, kuhakikisha hali inakua bora na hasa kuhakikisha vitendo vinakua vya muda mrefu. Haitoshi kutuma wasaidizi wa huduma za jamii mambo yanapoanza kutokota.Juhudi imara za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii zinabidi ziwe za muda mrefu.

Mwandishi: Fürstenau, Marcel (DW Berlin)/ Hamidou, Oummilkheir

Mpitiaji: Miraji Othman

 • Tarehe 03.09.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P3si
 • Tarehe 03.09.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P3si
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com