Mustakabali wa Somalia ukoje? | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mustakabali wa Somalia ukoje?

Nchini Somalia, hali inazidi kuwa mbaya tena. Kuna ripoti kadhaa kuhusu mashambulio ya makombora yaliyotokea Mogadishu na pia vizuizi vya mabarabarani vimejengwa upya. Mwezi moja na nusu baada ya jeshi la Ethiopia kuingilia Somalia ilionekana amani inarudi, lakini sasa inaelekea kuwa Somalia inarudi katika ghasia.

Mwanajeshi wa serikali ya Somalia mjini Mogadishu

Mwanajeshi wa serikali ya Somalia mjini Mogadishu

Haya pia ni maoni ya washiriki kwenye majadiliano yaliyofanyika hapa Deutsche Welle Bonn juu ya mustakabali ya Somalia na nguvu ya magaidi nchini humo.

Somalia inadhibitiwa tena na viongozi na makundi madogo madogo ya koo mbali mbali, na hivyo ni vigumu kwa jumuiya ya Kimataifa na Umoja wa Ulaya kutafuta wawakilishi wanaokubaliwa na wengi wa Wasomali, haya aliyasema Bibi Annette Weber wa taasisi maarufu ya uchunguzi wa mambo ya kisiasa na kisayansi mjini Berlin. Hata ndani ya Umoja wa Mahakama za Kiislamu makundi mbali mbali yametangana, kwa hivyo sasa inasemekana kuna makundi ya siasa za wastani, mengine ya siasa kali, na mengine ambayo yamejificha au kukimbilia nchi nyingine.

Lakini ushawishi ya ugaidi kutoka nje, anasema Bi Weber, hauhusiani na mwenendo huo: "Kusema kuwa hayo yanatokana na ushawishi wa Al Qaida au Majihadin kutoka nje, hayaambatani na hali halisi ya mambo nchini Somalia.”

Tofauti lakini ni maoni ya mtaalamu wa mambo ya Kiafrika wa chama cha Christian Demokrats katika bunge la Ujerumani, Bw. Hartwig Fischer: “Tumeambiwa na idara za usalama Al Qaida inazidi kuwa na nguvu katika eneo hili na kuwa kundi hili liliusaida Umoja wa Mahakama za Kiislamu kufanya harakati zake za kijeshi na kuzigharamia.”

Kwa sababu hiyo, Bw. Fischer anasisitiza umuhimu wa kushirikiana na Waislamu wasio na msimamo mkali na kuunda serikali mpya ya mpito inayoziunganisha koo zote za Somalia. Bi Annette Weber, vile vile, alikumbusha kwamba inabidi kuwa na mawazo juu ya utaratibu wa kuubalidisha mfumo wa kisiasa kabla ya kuingizwa jeshi la Umoja wa Afrika la kuhakikisha amani. Idadi ya wanajeshi walioahidiwa kupelekwa kwa ajili hiyo hadi sasa ni 4000, yaani nusu ya idadi iliyoamuliwa kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika. Wataalum wengi lakini wana wasiwasi juu ya uwezo wa jeshi kama hilo.

Pamoja na kutuma jeshi, ni muhimu kuendelea na jitihada za kidiplomasia, alisema mwanasiasa Hartwig Fischer: “Kulifanyika mazungumzo na Algeria na Libya. Lazima kujua kwamba tunajitahidi sana kupitia nchi hizi kwa sababu tunajua zina ushawishi mkubwa katika eneo hili.”

Aliyekosoa sera za Ujerumani kuelekea Somalia lakini ni Ulrich Delius wa shirika linalotetea haki za binadamu na kusema kuwa suala la pembe ya Afrika halipewi umuhimu katika wizara ya mambo ya kigeni. Naye alisema: “Bila shaka kuna mazungumzo mengi yanayofanyika kisiri, lakini tunataka kuona hatua halisi, kwani hiyo ni kuonyesha Somalia na Afrika nzima umuhimu gani tunaoutoa kutatua mizozo barani Afrika.”

Yaliyokubaliwa na waliohudhuria wote ni kwamba vita hivi visitajwe kuwa ni vita vya kidini, ama sivyo kuna hatari kubwa vita hivyo kuwa vikali zaidi.

 • Tarehe 07.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHKY
 • Tarehe 07.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHKY

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com