1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Serikali yatangaza muda wa kutotembea usiku

21 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBpg

Uongozi nchini Somalia unatangaza muda wa kutotembea wakati wa usiku mjini Mogadishu baada ya watu watatu zaidi kuuawa katika ghasia mjini humo.Kwa mujibu wa mkuu wa Shirika la Usalama wa Kitaifa Mohamed Warsame Darwish agizo hilo linaanza kutekelezwa hapo kesho kuanzia saa moja za jioni hadi kumi na moja alfajiri.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya watu watatu kupoteza maisha yao baada ya guruneti kulipuka kwenye soko la Bakara mjini Mogadishu.

Wiki jana polisi walitangaza muda wa kutotembea usiku mjini Baidoa baada ya maguruneti kulipuka kwenye ukumbi wa filamu na benki ya serikali.Shambulio hilo lilisababisha yapata watu watatu kuuawa na kujeruhi wengine zaidi ya kumi na mbili.

Ghasia zimeongezeka mjini Mogadishu tangu majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na majeshi ya Ethiopia kuwafurusha wapiganaji wa mahakama za kiislamu mwezi Aprili baada ya kipindi cha miezi kadhaa cha mapigano yaliyosababisha vifo vya mamia ya raia na maelfu kuachwa bila makao.

Wapiganaji wanalenga kuwashambulia maafisa wa serikali ,majeshi ya Ethiopia na majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika ili kukwamisha juhudi za kulinda amani nchini Somalia. Mazungumzo ya amani yanayounaoungwa mkono na Umoja wa mataifa yanayolenga kuleta pamoja vikundi vinavyohasimiana yaliahirishwa tena kwa mara ya tatu hadi katikati ya mwezi ujao kwasababu za kiusalama na ukosefu wa fedha.