Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa waanza Bonn | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 30.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa waanza Bonn

Marekani imejitolea kwa dhati kutafuta mkataba mpya wa kimataifa

Yvo de Boer katibu wa sekretariati ya Umoja wa Mataifa ya hali ya hewa

Yvo de Boer katibu wa sekretariati ya Umoja wa Mataifa ya hali ya hewa

Mkutano wa kimataifa unaojadili mabadiliko ya hali ya hewa unaendelea hapa mjini Bonn Ujerumani. Mkutano huo ulionza jana Jumapili unafuatia mkutano wa Disemba mwaka jana uliofanyika mjini Copenhagen Danemark. Mazungumzo yanatarajiwa kuendelea kwa muda wa siku 11.

Serikali ya Marekani inashiriki kikamilifu kwenye mazungumzo yanayolenga kuandaa mkataba wa kimataifa kuhusu hali ya hewa, lakini peke yake haiwezi kuuokoa mchakato huo unaokabiliwa na matatizo. Hayo yamesemwa na mjumbe wa Marekani anayehusika na maswala ya hali ya hewa, Todd Stern, kwenye mkutano wa kimataifa unaojadili mabadiliko ya hali ya hewa unaondelea hapa mjini Bonn.

Kushiriki kwa Marekani kwenye mazungumzo yanayozijumulisha zaidi ya nchi 190 na zinazokabiliwa na mpasuko mkubwa kati ya nchi tajiri na nchi zinazoendelea, kumezusha matumaini makubwa tofauti kabisa na utawala wa rais George W Bush. Kiongozi huyo aliupinga mkataba wa Kyoto ambao mamlaka yake inamalizika mwaka 2012 na pia akakaribia kuyavuruga makubaliano ya Bali ya mwaka 2007 yaliyoweka mwezi Disemba mwaka 2009 kuwa tarehe ya mwisho ya kuundwa mkataba mpya.

Akiwahutubia wajumbe zaidi ya 2,500 kwenye ufunguzi wa mkutano wa Bonn, mjumbe wa Marekani, Todd Stern, amesema Marekani inafuraha imerejea kwenye mazungumzo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Matamshi yake yalishangiliwa na idadi kubwa ya wajumbe, hata wale kutoka mataifa ambayo bado yanaukosoa mpango wa rais wa Marekani Barack Obama kuhusu hali ya hewa.

Mkutano wa Bonn ni raundi ya kwanza kati ya raundi tatu za mazungumzo zinazofuatia mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa uliofanyika Copenhagen nchini Denmark. Kiongozi wa sekretariati ya Umoja wa Mataifa inayohusika na hali ya hewa, Yvo de Boer, anasema kufikia mwezi Juni mwaka huu, wakati mkutano mwingine utakapofanyika hapa Bonn, lazima kuwe na rasimu ya mkataba mpya wa kimataifa wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Mpaka sasa Japan na Urusi hazijawasilisha malengo yao ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Kutoka Japan na Urusi mpaka sasa bado hatujapokea lengo lililo wazi. Haijabainika wazi vipi pesa zitakavyotolewa. Kwa nchi nyingi zinazoendelea, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ni swala la umuhimu mkubwa."

Wanaharakati wa kulinda mazingira wameeleza matuimaini yao kuhusu mkutano wa Bonn. Martin Kaiser wa shirika la kulinda mazingira la Greenpeace la hapa Ujerumani anauona mgogoro wa kiuchumi kama nafasi ya kuwekeza katika nishati inayoweza kutumiwa upya.

"Mgogoro wa kiuchumi sasa unatoa fursa kubwa kutumia fedha za serikali kuwekeza katika nishati inayoweza kutumiwa upya na kuondokana na teknolojia ya zamani iliyopitwa na wakati ya kutumia makaa ya mawe na nyuklia."

Hii leo Umoja wa Ulaya umeupongeza mualiko wa rais wa Marekani Barack Obama kwa mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa kwa nchi zilizoendelea kiuchumi duniani, pamoja na hatua yake ya kuondokana na sera za rais Bush aliyekosolewa kwa kuzuia juhudi za kukabiliana na ongezeko la ujoto duniani. Kamishna anayehusika na uhusiano wa kigeni katika Umoja wa Ulaya, Benita Ferrero-Waldner, amesema akiwa ziarani Beijing China kwamba mkutano wa nchi 16 zilizoendelea kiuchumi duniani utakaofanyika mwezi ujao mjini Washington ni pendekezo zuri.

Marekani imejitolea kwa dhati kuhakikisha mkataba wa hali ya hewa unapatikana, lakini imezitaka nchi nyingine zisaidie.


Muandishi: Guarino, Monika/Charo

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 30.03.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HMev
 • Tarehe 30.03.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HMev
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com