1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa SADEC kuhusu Zimbabwe

Thelma Mwadzaya27 Januari 2009

Viongozi wa Jumuiya ya maendeleo ya SADC wamewaagiza Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na hasimu wake wa kisiasa Morgan Tsvangirai kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa kabla kufikia katikati ya mwezi wa Februari.

https://p.dw.com/p/GgxP
Morgan Tsvangirai na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.Picha: AP

Kauli hiyo imetolewa baada ya kukamilika kwa mkutano wa dharura wa siku mbili mjini Pretoria.Lengo la kikao hicho kilikuwa kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaokumba nchi ya Zimbabwe hata baada ya mwafaka wa kugawana madaraka kufikiwa Septemba iliyopita.Uchaguzi mkuu uliogubikwa na utata ulifanyika mwezi Machi mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa Katibu mtendaji wa Jumuiya ya SADC Tomaz Salomao kiongozi wa Upinzani Morgan Tsvangirai ataapishwa rasmi ifikapo tarehe 11 mwezi Februari mwaka huu ili aweze kutekeleza majukumu yake ya uongozi kwa ushirikiano na Rais Robert Mugabe.Mawaziri wanatarajiwa kuapishwa siku mbili zitakazofuatia hatua itakayokamilisha uundwaji wa serikali inayoshirikisha pande zote.Kikao hicho cha dharura kilichukua muda wa saa 14.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa nchini Zimbabwe yaliyofanyika mjini Harare yaliambulia patupu.Zimbabwe inazongwa na mkwamo wa kiuchumi kadhalika baa la ugonjwa wa kipindupindu kilichosababisha vifo vya yapata watu alfu 2800 tangu kuzuka mwezi Agosti mwaka uliopita.Rais Robert Mugabe na hasimu wake wa kisiasa Morgan Tsvangirai walifikia mwafaka wa kugawana madaraka mwezi Septemba mwaka uliopita, hatua iliyokabiliwa na mivutano na tofauti kuhusu nyadhifa nyeti serikalini.

Mwenyekiti wa zamu wa Jumuiya ya Maendeleo ya SADC Kgalema Motlanthe aliye pia rais wa Afrika Kusini ana imani kuwa mahasimu hao watatimiza kilichoafikiwa ifikapo tarehe hiyo.

Chama tawala kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe kilitosha kuunda serikali mpya hata bila ushirikiano wa upande wa upinzani.

Wasuluhishi wa pande zote mbili wanatazamiwa kukutana hivi punde kwa lengo la kujadili mswada wa baraza la usalama wa kitaifa uliowasilishwa na chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC.Mkutano huo pia unatazamia kujadili mfumo maalum wa kuteua magavana kama ilivyoagiza Jumuiya ya SADC.

Kwa upande mwengine Jumuiya ya SADC imeamua kuwa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani sharti yagawanywe kati ya upinzani na chama tawala vilevile kudurusiwa baada ya kipindi cha miezi sita ya serikali mpya kuwa madarakani.Agizo hilo limepingwa vikali na chama cha MDC.

Kulingana na kiongozi wa upinzani wa chama cha Movement for Democratic Change MDC Morgan Tsvangirai maazimio hayo mapya hayajawafurahisha.Kiongozi huyo amesisitiza kuwa hatua ya kuunda serikali inayokubalika ndio mkondo wa kufuata.

Chama cha MDC kimetangaza kuwa kitatangaza msimamo wake kuhusu suala hilo baada ya baraza lake la kitaifa kukutana mwishoni mwa juma hili.

Kulingana na Jumuiya ya SADC masuala mengine yanayohusiana na mamlaka ya Rais Mugabe yanaripotiwa kuwa yatajadiliwa.Chama cha MDC kimekuwa kikishikilia kuwa sharti wafuasi wake wanaozuiliwa jela waachiwe huru kabla ya wao kuingia serikalini.

Kikao hicho cha dharura kilikuwa cha tatu kufanyika chini ya uenyeji wa SADC katika kipindi cha mwaka mmoja.Kabla ya mazungumzo hayo kuanza Umoja wa Ulaya uliuwekea uongozi wa Zimbabwe mbinyo zaidi kwasababu ya kukidhi mahitaji ya raia wake vilevile kukiuka hakli za binadamu.

Katika masuala ya uchumi Zimbabwe inakabiliwa na mparaganyiko mkubwa huku mfumko wa bei za bidhaa ukiripotiwa kupita asilimia 230.Shughuli zote za biashara nchini humo zinatimizwa kwa kutumia sarafu ya dola kwani thamani ya sarafu ya Zimbababwe inaporomoka kila uchao.Hata hivyo wadadisi wanaonya kuwa matumizi ya dola ni suluhu ya muda mfupi.Kwa sasa wafanyabiashara wengi wanatumia dola za marekani,paundi ya Uingereza,rand ya Afrika Kusini vilevile pula ya Botswana kununua na kuuza bidhaa.

Uchumi wa Zimbabwe unaripotiwa kunywea kwa yapata asilimia 40 katika kipindi cha miaka 6 iliyopita.Kipindi kirefu cha ukame nacho pia kinazidi kutatiza hali iliyopo nchini humo.

RTRE

DPAE

AFPE