1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya wafanyika Luxembourg

Josephat Charo23 Aprili 2007

Mazungumzo baina ya Umoja wa Ulaya na Iran yanataraji wa kufanyika nchini Uturuki wiki hii.

https://p.dw.com/p/CHFe
Kiongozi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana
Kiongozi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier SolanaPicha: picture alliance / dpa

Umoja wa Ulaya umekubali kukutana na Iran huku mawaziri wa mashauri ya kigeni wa umoja huo wakikubaliana kuiwekea Iran vikwazo vya kuibinya iachane na urutubishaji wa madini ya uranium. Kiongozi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, amesema leo mjini Luxembourg kwamba atakutana na mpatanishi wa Iran katika mzozo wa nyuklia, Ali Larijani, kesho kutwa Jumatano mjini Ankara nchini Uturuki. Lengo la mkutano huo ni kuishawishi Iran ikubali kuendelea na mashauriano.

´Natarajia kuanza tena mazungumzo kutoka mahali tulipofikia mara ya mwisho ili tuone kama tutaweza kusonga mbele na kufikia mashauriano.´

Mawaziri wote 27 wa mashauri ya kigeni wameongeza mbinyo wa Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran kwa kukubaliana juu ya vikwazo vitakavyotekelezwa kupita mwezi Disemba, tarehe ya mwisho ya vikwazo vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Mawaziri hao pia wameongeza orodha ya majina ya watu na mashirika yanayohusika na mpango wa nyuklia wa Iran, hivyo kuongeza majina katika orodha iliyotolewa na Marekani.

Katika mkutano mjini Luxembourg, Umoja wa Ulaya umeanzisha mpango wa kulisadia bara la Afrika kujenga miundombinu yake ikiwa ni pamoja na barabara, reli, nishati, mifumo ya kusambaza maji na mitandao ya mawasiliano ya simu. Mpango huo utagharimu euro milioni 347. Benki ya uwekezaji ya Ulaya, ambayo ni kitengo cha kutoa mikopo cha Umoja wa Ulaya, itatoa mikopo ya kiwango cha euro milioni 260 kwa kiwango cha chini cha riba.

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imesema kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa leo mjini Luxembourg, mikopo hiyo italenga miradi mbalimbali barani Afrika. Halmashauri hiyo pamoja na Austria, Belgium, Italy, Uhispania, Luxembourg na Uholanzi zitatoa euro milioni 87 kama mikopo.

Umoja wa Ulaya pia umerefusha muda wa vikwazo dhidi ya Zimbabwe kwa mwaka mwingine mmoja, huku ukipanua marufuku ya ziara za rais Robert Mugabe na mawaziri wake serikalini. Taarifa iliyotolewa na mawaziri wa kigeni wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg haikutaja majina yatakayoongezwa kwenye orodha ya majina ya viongozi waliopigwa marufuku kuingia Ulaya.

Hatua hiyo imekwamisha mpango wa Umoja wa Ulaya kuandaaa mkutano na viongozi wa Afrika, lakini Ureno imesema ina matumaini kuandaa mkutano baina ya Umoja wa Ulaya na Afrika wakati itakapochukua urais wa umoja huo kutoka kwa Ujerumani.

Kuhusu serikali ya mamlaka ya Palestina, Umoja wa Ulaya umeendelea kushikilia msimamo wake wa kukatisha misaada ya Umoja kwa moja kwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa lakini ukaapa kushirikiana kwa karibu na mawaziri wasio wanachama wa chama cha Hamas ili kupunguza hali ngumu ya kiuchumi katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa magharibi wa mto Jordan.