Mkutano wa kuisadia Somalia wamalizika Madrid | Habari za Ulimwengu | DW | 29.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

Mkutano wa kuisadia Somalia wamalizika Madrid

Mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Taasisi ya International Somalia Contact Group (ISCG) umemalizika jana mjini Madrid ukiitolea wito jumuiya ya kimataifa iisaidie Somalia kupambana na tatizo la uharamia

Sasa jumuiya ya kimataifa inaanza kutambua kwamba, haiwezi kumaliza tatizo la uharamia dhidi ya meli za kigeni katika bahari ya Somalia, kwa kuongeza boti za doria peke yake, bali kwa kukitibu chanzo cha kuwepo kwa uharamia huo.

Huo ndio muakisiko wa mkutano wa kimataifa juu ya Somalia uliomalizika jana nchini Hispania, ambapo imekubaliwa kwamba sasa kutumike njia mbadala ya kuwageuza watekaji meli kuwa wavuvi. Hispania, iliyokuwa mwenyeji wa mkutano huo, imejibebesha jukumu la kuonesha njia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Hispania, Miguel Angel Moratinos, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba lengo la nchi yake kufanya hivyo ni kutumia uzoefu wake katika masuala ya uvuvi ili kuisaidia sekta ya uvuvi nchini Somalia iwe na uwezo wa kutumia rasilimali zake kwa manufaa ya nchi.

Mkutano huu uliohudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 45 na mashirika ya kimataifa, uliitishwa ili kuiangalia upya hali ya Somalia, ambayo wachunguzi wa mambo wanasema imedharauliwa na kusahauliwa na jumuiya ya kimataifa.

Waziri Moratinos alisema kwamba, nchi yake inataka kuwageuza maharamia wa Somalia kuwa wavuvi, kwani taarifa za kiusalama zinaonesha kuwa wengi wa maharamia wanaokamatwa, hubainika kwamba ni wavuvi wa kawaida, ambao wameachana na uvuvi na kujiingiza katika uhalifu huu, baada ya bahari yao kuvamiwa na meli kubwa za kigeni zinazovua kinyume na sheria.

Somalia, ambayo imekuwa haina serikali madhubuti kwa miongo miwili sasa, ina eneo refu zaidi la bahari katika pembe ya Afrika, na bahari hiyo ni maarufu kwa samaki wake aina ya nguru, jodari, taa na saadini, ambao huuzwa kwa bei kubwa katika nchi za Ulaya na Marekani. Meli kubwa za nchi za Korea ya Kusini, Japan na Hispania ni miongoni mwa vyombo vinavyotajwa na taarifa ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2006, kuonekana vikiendesha uvuvi haramu katika eneo hilo, vikitumia fursa ya kutokuwepo kwa jeshi la wanamaji la Kisomali.

Mkutano huu wa Madrid, ambao pia ulihudhuriwa na Rais wa Serikali ya Mpito ya Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, uliitaka jumuiya ya kimataifa kuiangalia Somalia sawa sawa na inavyoziangalia nchi za Iraq na Afghanistan. Washiriki walisema kwamba, Somalia haitaki tu msaada wa kifedha, lakini inahitaji pia dhamira ya kweli ya kisiasa kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Sasa maazimio ya mkutano huu wa Madrid, yanajenga matumaini kwamba bahari ya Somalia inaweza ikawa salama, sio tu kwa kuepukana na uharamia, bali pia kwa kutokuwepo meli za kigeni zinazopora maliasili ya nchi hiyo masikini iliyoraruliwa na miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 29.09.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PPbd
 • Tarehe 29.09.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PPbd
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com