Mkutano wa G20 umemalizika | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 12.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mkutano wa G20 umemalizika

Sheria kali za kusimamia taasisi za fedha diniani zimeidhinishwa na viongozi wote

default

Viongozi wa kundi la G20 katika mkutano wa Seoul, Korea Kusini

Viongozi wa nchi za kundi la G20 leo wameidhinisha sheria kali za kusimamia Taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na kupitisha sheria zitakazoangalia viwango vya pesa katika Mabenki ili kuzuia hatari ya kutokea tena mporomoko wa kiuchumi duniani.

Viongozi hao wa kundi la G20 wamekamilisha mkutano wao wa kilele mjini Seoul hivi punde kwa kupitisha azimio linalounga mkono hatua za kuboresha  taasisi kubwa za fedha duniani,ambazo zimekuwa zikionekana haziwezi kupata matatizo ya kiuchumi.

Katika taarifa ya viongozi hao wamesema kwamba mpango mpya uliokubaliwa utahakikisha kwamba mfumo wa fedha unadhibitiwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzoni kwa lengo la kuimarisha uchumi wa dunia.

G20 G-20 Seoul Sitzungssaal NO FLASH

Wakuu hao wa nchi tajiri wamejadiliana katika kikao cha siku mbili kuhusu kisomo walichokipata kutokana na mporomoko wa masoko ya fedha duniani ulioshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni, ambapo pia wamezungumzia suala la kuwepo haja ya kupunguza kitisho cha kuanguka kwa mabenki makubwa duniani na kusababisha mtikisiko wa kiuchumi.

Wamekiri katika kikao hicho kwamba ulimwengu umejifunza kisomo kikubwa baada ya kuporomoka kwa benki ya Lehman Brothers ya Marekani mwaka 2008, hali iliyosababisha mshutuko mkubwa wa kiuchumi kote duniani. Akizungumza hivi punde rais Obama amesema.

''Tulikuja Seoul kuendeleza kazi iliyotupeleka kuanzia London, Pittsburg hadi Toronto.Tuatashirikiana kuukwamua uchumi wa dunia kutoka kwenye janga kubwa.Tunataka kuepuka mporomoko wa masoko ya fedha kulikosababisha kuanguka kwa uchumi wa dunia. Tumeamua kuzingatia mizani sawa katika kuukuza na kuuendeleza uchumi. Pia tumekubaliana juu ya mpango wa kuchukua hatua katika kukabiliana na rushwa''

Viongozi wa G20 wamesema kwamba hatua hiyo ya kuyadhibiti mabenki na taasisi za fedha imetokana na hali iliyoshuhudiwa mwaka 2008 ya kutowajibika kwa viongozi wa vyombo hivyo pamoja na kuwepo dosari kubwa katika sheria na usimamizi wa Mabenki hayo.

G20 Seoul Merkel / Berlusconi / Sarkozy

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy,Kulia, Waziri mkuu Silvio Berlusconi, Kushoto na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Ama kwa upande mwingine, nchi zenye nguvu katika Umoja wa Ulaya, Uingereza Ufaransa, Ujerumani, Itali na Spain zimetoa taarifa ya pamoja katika mkutano huo wa Seuol zikisisitiza kwamba mpango mwingine wa kuupiga jeki uchumi unaweza tu kufanyika katikati ya mwaka 2013 bila ya kuathiri mipango ya wakati huu.

Aidha Kansela Merkel amezungumzia pia wasiwasi uliopo kuhusiana na ati ati za Ireland kujikuta katika mporomoko wa kiuchumi. Amesema walipa Kodi wa nchi za Ulaya hawapaswi kubeba mzigo wa kulipia gharama zote  za kuziokoa nchi zinazozongwa na madeni. Lakini  kwa mujibu wa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, Umoja huo umejiandaa kuisaidia mkono Ireland.

Mkutano mwingine wa G20 umepangwa kufanyika Ufaransa mwakani ambapo tayari rais Nicolas Sarkozy ameshawaalika viongozi wa kundi hilo katika mji wa Cannes.

Mwandishi Saumu Mwasimba/APE

Mhariri Othman Miraji

 • Tarehe 12.11.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Q6lm
 • Tarehe 12.11.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Q6lm

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com