Mkutano wa EU na China wamalizika patupu | Habari za Ulimwengu | DW | 07.10.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Mkutano wa EU na China wamalizika patupu

Mkutano wa kutafuta suluhu kwenye masuala ya kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya na China umemalizika bila ya kufikiwa kwa makubaliano yoyote

Kutoka kushoto, Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy, Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao, Mfalme wa Ubelgiji Albert II, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Yves Leterme na Rais wa Kamisheni ya Ulaya Jose Manuel Barroso

Kutoka kushoto, Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy, Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao, Mfalme wa Ubelgiji Albert II, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Yves Leterme na Rais wa Kamisheni ya Ulaya Jose Manuel Barroso

Mwanzoni mwa mkutano huu, Rais wa sasa wa Jumuiya ya Ulaya Herman Van Rompuy, alionesha matumaini kwamba, licha ya tafauti zilizopo kati ya Ulaya na China, mkutano wao ungemalizika kwa makubaliano yenye maslahi kwa pande zote mbili, kwani kila upande una maslahi yake kwa mwengine.

Van Rumpoy alisema kwamba, kama ulivyo ushirikiano wowote wa kikweli, China na Ulaya nazo zina mambo yanayozikutanisha pamoja na yale yanayowatafautisha.

"Lakini hilo halipaswi kuzizuwia jitihada zetu za kuyapandisha mahusiano yetu kwenye kiwango cha juu. Lazima tuwe na dhamira ya kuendeleza mahusiano na tufanye juhudi za makusudi kutimiza dhamira hiyo." Alisema Van Rumpoy.

Matumaini haya pia yalionekana upande wa China. Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, ambaye ni mara yake ya nane kushiriki kwenye mkutano kama huu, aliamini kwamba tafauti za miaka ya nyuma zingeliweza na kusuluhishwa, kwani kwa upande mmoja Umoja wa Ulaya ni Jumuiya yenye uchumi mkubwa na kwa upande mwengine China ni nchi yenye uchumi mkubwa pia.

"Mahusiano ya kiuchumi baina ya Ulaya na China ni kitu chenye manufaa. Daima China imedhamiria kufanya kila lililo kwenye uwezo wake, kuyalinda na kuyadumisha mahusiano haya." Alisema Wen Jiabao.

Lakini jana, mkutano huu ukamalizika, bila ya matarajio haya kutimizwa. Kila upande ukaondoka mkutanoni hapo mikono mitupu. Kwa mujibu wa vyanzo vya Umoja wa Ulaya, masuala yaliyozifanya pande hizi mbili kuondoka Brussels bila kukubaliana ni yale yanahohusiana na biashara na haki za binaadamu.

Baada ya kumalizika mkutano, hakukuwa na mazungumzo rasmi na vyombo vya habari, kama ilivyo ada ya mikusanyiko, huku mwanadiplomasia mmoja kwenye mkutano huo, akinukuliwa na Shirika la Habari la AFP akisema kwamba, washiriki wa mkutano waligundua wakiwa kwenye mazungumzo kwamba wasingelikuwa na kikubwa cha kuwaeleza waandishi.

Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jean-Manuel Barroso, alisema palikuwa na mjadala wa wazi kuhusiana na suala la haki za binaadamu, ambayo ni mada inayopendwa sana na Ulaya inapokutana na China, lakini daima limekuwa halizikutanishi pande hizi mbili. Juhudi za Umoja wa Ulaya kulifanya taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi la China kukubaliana na viwango vya kimataifa vya haki za binaadamu hazikufanikiwa.

Hata hivyo, inaonekana kwamba kumalizika kwa mkutano huu bila ya mafanikio, hakukufunga milango ya mafanikio mengine baina ya nchi moja moja za Ulaya na China. Baada ya kumalizika tu kwa mkutano huo, Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabhao alipanda ndege na kuelekea Italia, ambako alitarajiwa kuweka saini mkataba wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili wenye thamani ya Euro bilioni mbili na nusu.

Vyombo vya habari vya Italia vinasema kwamba mkataba huu utajumuisha mradi wa kujenga kinu cha kuzalishia umeme wa jua nchini Italia wenye thamani ya dola milioni nane za Kimarekani na pia mikataba miwili ya kusambaza huduma ya mtandao wa Intaneti nchini humo.

Baadaye leo hii, Wen Jiabao anatarajiwa kuwasili nchini Uturuki kwa ujumbe huo huo wa kibiashara kati ya nchi hizi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com