Mkutano wa dharura waidhinisha mkopo kwa Ugiriki
8 Mei 2010Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema kundi hilo la mataifa 16, litatoa ujumbe maalum kwa walunguzi, kwa kuanzishwa mfuko maalum wa dharura, kwa azma ya kuzuia matatizo ya deni katika mataifa mengine ya Ulaya.
Serikali ya Ugiriki imechukua jukumu la kubana matumizi yake katika jitahada za kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ili nchi hiyo iweze kupata mikopo ya dharura kutoka nchi za kanda ya euro na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.
Hatua hiyo ya serikali ya Ugiriki imepingwa vikali na raia nchini humo. Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou alipozungumza mjini Brussels alisema sio nchi yake pekee inayokabiliwa na matatizo ya deni.
Nchini Ujerumani, wabunge mjini Berlin, wameidhinisha mswada wa sheria inayofungua njia ya kuipatia mkopo Ugiriki. Rais wa Ujerumani, Horst Köhler ametia saini mswada huo kuwa sheria.
Kuambatana na makubaliano ya mkopo huo, Ujerumani itaipatia Ugiriki Euro bilioni 22. Ujerumani inatoa sehemu kubwa ya mkopo unaotolewa na nchi zinazotumia sarafu ya Euro, kwa sababu pia ni nchi iliyo na uchumi mkubwa kabisa katika kundi la mataifa 16 yanayotumia Euro.
Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE
Mhariri:P.Martin