1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Commonwealth wamalizika

Josephat Charo26 Novemba 2007

Mkutano wajumuiya ya madola, Commonwealth, umemalizika leo mjini Kampala Uganda. Mjadala umetuwama juu ya njia za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/CT1Z
Rais Yoweri Museveni wa Uganda (kulia) na malkia Elizabeth II wa UingerezaPicha: AP

Mkutano wa kilele wa viongozi wa taifa na serikali wa jumuia ya madola, Comonwealth, ulioanza Ijumaa iliyopita, umemalizika hivi punde katika mji mkuu wa Uganda Kampala baada ya mijadala kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na kanuni za biashara ya kimataifa.

”Mkutano wa kilele umemalizika,” amesema rais Yoweri Museveni wa Ugada katika sherehe za kuufunga mkutano huo, zilizofanyika katika hoteli moja mashuhuri nje ya mji mkuu wa Uganda, Kampala.

Taarifa ya pamoja iliyotangazwa leo na kuvifikia vyombo vya habari, inakumbusha maadili ya kimsingi ya jumuia ya Commonwealth na kugusia masuala kuhusu kwa mfano upunguzaji wa silaha, ugaidi, haki za binaadam, biashara na ukimwi.

Viongozi walishindwa hapo jana kuafikiana juu ya msimamo wa pamoja dhidi ya kuchafuliwa hali ya hewa na namna ya kupunguza moshi wa viwandani.

Jana viongozi wa jumuiya ya madola, Commonwealth, walimchagua balozi wa India nchini Uingereza, Kamalesh Sharma, kuwa katibu mkuu mpya. Atakabidhiwa wadhifa huo April mwakani wakati Don McKinnon wa kutoka New-Zealand atakapomaliza mihula miwili ya wadhifa huo wa miaka minne.

Mkutano wa mwaka huu wa jumuiya ya madola Commonwealth uligubikwa na kusitishiwa uanachama Pakistan na baraza la mawaziri. Hii ni mara ya pili kwa Pakistan kusimamishiwa uanachama baada ya kuachwa nje kwa muda wa miaka mitano baada ya mapinduzi yaliyomleta madarakani Pervez Musharaf mnamo mwaka 1999.