Viongozi wa Umoja wa Ulaya wajadili nishati na mabadiliko ya hali ya hewa
13 Machi 2008
Viongozi wa nchi na serikali wa Umoja wa Ulaya leo wanakutana kwenye makao makuu ya Umoja wao,mjini Brussels kujadili masuala ya usalama wa nishati, mabadiliko ya hali ya hewa na mageuzi katika nchi zao.
Viongozi hao kutoka nchi 27, kwenye mkutano wao pia watajadili suala la umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterania litakalowasilishwa kwa pamoja baina ya raisNicolas Sarkozy wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Ujerumani na Ufaransa ziemeweka kandoa tofauti zao juu ya suala hilo kufuatia mkutano wa viongozi wa nchi hizo wa hivi karibuni.
Lakini awali ya yote mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya unaotarajiwa kuendelea hadi kesho utajadili masuala ya usalama wa nishati na mabadiliko ya hali ya hewa.
Nchi za Umoja huo zinaazimia kusimama safu ya mbele katika juhudi za kupunguza utoaji wa gesi zinazoathiri mazingira.
Viongozi kutoka nchi 27 za Ulaya watapokea taarifa inayotahadharisha jinsi amani ya dunia inavyohatarishwa. Taarifa hiyo pia inatabiri wimbi kubwa la wakimbizi kutoka barani Afrika na kutoka mashariki ya kati kuanzia mwaka wa 2010.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya kwenye mkutano wao pia watajadili namna ya kuelekeza uhusiano wa nchi zao na Serbia baada ya Kosovo kujitangazia uhuru hivi karibuni.