Mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya: Faida au Athari? | Magazetini | DW | 25.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya: Faida au Athari?

Baada ya kufikiwa makubaliano kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa juma lililopita, sifa kwa kansela Angela Merkel wa Ujerumani ni nyingi. Licha ya mvutano mkubwa kati ya nchi wanachama juu ya mkataba mpya wa Umoja huu, Bi Merkel aliweza kuzipatanisha pande zote. Poland ilitishia kuzuia makubaliano ikipinga utaratibu mpya wa kupiga kura ambao utaahirisha kwa miaka mitano na kuanza kutumika mwaka 2014 tu.

Maoni ya wahariri wa Ujerumani juu ya suala hilo ni tofauti. Kwanza ni gazeti la “Hamburger Abendblatt”:

“Ujeuri unashinda. Hilo ni funzo baada ya mazungumzo marefu ya mkutano huu wa Umoja wa Ulaya. Uingereza ulisisitiza juu ya wasiwasi wake kuhusu Umoja wa Ulaya wenye nguvu mkubwa mno na Poland pia ilirudia tisho lake hadi makubaliano yalipopatikana ambayo yaliziridhisha Poland, Uingereza na nchi nyingine. Basi ikiwa unaendelea kulalamika tu, hatimaye utapata yale unayoyataka. Wale lakini wanaosaidia kujenga Umoja huu na kufuata sheria, hawapati faida.”

Kulingana na mhariri wa “Rhein-Zeitung”, mkataba huu mpya ni mwanzo tu wa njia ndefu. Ameandika:

“Viongozi hao 27 waliweka msingi kwa ushirikiano utakaokuwa na nguvu zaidi, yaani katika vita dhidi ya ugaidi Umoja huo utaweza kuchukua hatua, utaweza kutekeleza mradi wake wa kulinda mazingira, kukabiliana na changamoto katika enzi hii ya utanda wazi na kuziunganisha nchi nyingi zaidi katika Umoja huu. Lakini mkataba huo haumaanishi sera bora, kwani la muhimu ni nia ya kushirikiana kisiasa. Kuhusiana na nia hiyo lakini kuna wasiwasi tukikumbuka vile nchi wanachama zilivyosisitiza maslahi yao ya kitaifa kwenye mkutano huo wa Brussels. Kwa hivyo, bado njia ni ndefu.”

Ni gazeti la “Rhein-Zeitung”. Mhariri wa “Flensburger Tageblatt” ana mwito mwingine:

“Tafadhalini, msidumishe faida ya mkutano huo wa kilele. Ndiyo, ilibidi kubadilisha mkataba ili kuishawishi Poland ikubali. Lakini tatizo hilo la kupima kura za nchi wanachama si kubwa sana. Muhimu zaidi ni kitu kingine, yaani kwamba Umoja wa Ulaya umemaliza mzozo huu juu ya katiba. Sasa si lazima tena ujishughulishe na masuala ya ndani tu. Licha ya maslahi yaliyokuwa tofauti sana, nchi hizo 27 wanachama ziliweza kupata muafaka. Ilikuwa kazi kubwa iliyoleta maumivu fulani, lakini ilifaulu.”

Na hatimaye kuhusu mkutano wa Umoja wa Ulaya na mkataba mpya, yafuatayo ni maoni ya gazeti la “Nordbayerischer Kurier”:

“Yaliyoonekana kwenye mkutano huo wa Brussels ni jeruhi za zamani za nchi za Ulaya Mashariki. Karibu, Kansela Merkel apoteze subira katika mazungumzo na Poland. Lakini alijikaza. Sisi sote tunapaswa tujikaze badala ya kukasirika juu ya madai ya Poland au Uingereza. Kwa kweli, ni sifa ya Ulaya kwamba tofauti kati ya nchi wanachama zinazingatiwa na kuheshimika. Ni ishara ya kwamba Umoja huu hautakuwa mamlaka mengine yanayotaka kuitawala dunia nzima.”

 • Tarehe 25.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSc
 • Tarehe 25.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSc