Mkakati mpya wa Afghanistan una uhakika? | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.12.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkakati mpya wa Afghanistan una uhakika?

Jana rais wa Marekani amewafahamisha wananchi wa Marekani kuhusu mkakati wake kuelekea Afghanistan.

Rais Obama akiwa katika Kituo cha kijeshi,Newyork

Rais Obama akiwa katika Kituo cha kijeshi,Newyork

Katika hotuba yake aliyoitoa katika chuo cha kijeshi cha West Point mjini New York , rais wa Marekani Barack Obama jana aliwafahamisha wananchi wa nchi hiyo , ni vipi mkakati wa kuongeza majeshi ya Marekani nchini Afghanistan utakavyokuwa. Suala la msingi ni kuhusu majeshi ya Marekani ambayo hadi hivi sasa yana wanajeshi wapatao 68,000, litaweza kuongezewa nguvu ya wanajeshi 30,000. Hatua hiyo ya kuliongeza jeshi la Marekani itakamilika katika majira ya joto mwakani . Mwaka mmoja baadaye , Julai 2011, uondoaji wa majeshi hayo kutoka Afghanistan utaanza kwa awamu , baada ya kulipatia uwezo jeshi pamoja na polisi wa Afghanistan kuweza kuchukua binafsi jukumu la ulinzi wa nchi hiyo. Ni kwa muda gani awamu hii itafanyika na haraka kiasi gani uondoaji wa majeshi utafanyika , itategemea zaidi hali katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo, amesema rais wa Marekani.

Kugusa kila upande

Barack Obama ni mtu wa kupenda maridhiano. Hilo mara nyingi ni jambo jema. Katika baadhi ya nyakati hata hivyo msimamo wa kati kwa kati ni chaguo baya kabisa. Kama ilivyo kwa Afghanistan. Rais anataka wanajeshi wa ziada 30,000 wapelekwe huko haraka iwezekanavyo na baada ya mwaka mmoja tu anataka waondolewe. Anataka kugusa kila upande. Kwa upande mmoja anapinga vita, kwa upande mwingine anajaribu pia kuhamasisha washirika wake kupambana na kundi la kigaidi la al-Qaeda na Taliban na kuyaendesha mapambano hayo kutokea mbali.

Kwa hali hiyo ya shaka shaka hayuko sahihi. Kwa wale wasiopendelea vita , kurefusha mapambano ya silaha kwa muda wa miaka miwili tayari ni muda mrefu sana. Kwa wale wakosoaji wake, kuweka muda wa kuyaondoa majeshi, hakutoshi, kwamba hakuna muda maalum uliowekwa na ni haraka kiasi gani kuweza kuyaondoa majeshi hayo. Kuna muda mfupi sana katika kupeleka na kuyaondoa kama vile rais anavyotaka kuwapeleka wanajeshi 30,000, tayari itakuwa changamoto kubwa sana kwa jeshi kwa utaratibu wa ugavi na usafirishaji wa watu na vifaa.

Kwa muda wa mwaka mmoja kuweza kufanya mambo mengi kwa pamoja ni muda mfupi sana, kuwaweka wanajeshi na wakati huo huo kuweza kupambana na al-Qaeda na kuwashinda, kulijenga jeshi la Afghanistan pamoja na kuwalinda raia itakuwa si rahisi.

Ridhaa ya Afghanistan

Na hili hata kwa rais binafsi liko wazi. Kuyaondoa majeshi kutategemea hali iko vipi nchini Afghanistan. Kwa hiyo muda uliowekwa wa kuyaondoa majeshi si wa kweli.Pamoja na hayo hotuba ya rais Obama inabaki katika vipengee kadha bila ya kuhafamika.

Kwa mwaka mwanajeshi mmoja anagharimu kiasi cha dola milioni moja nchini Afghanistan. Hakuna kilichoelezwa kuhusu hilo, ni vipi gharama ya ongezeko la wanajeshi litagharamiwa. Suala la kodi ya vita, kama ambavyo wengi wanaizungumzia , rais hakulitamka.Tamko la ukali dhidi ya utawala uliojaa ufisadi na usioweza kazi nchini Afghanistan halikutoka kinywani mwa rais.

Obama alifafanua kuwa haitakuwa rahisi tena kuuachia utawala huo wa Afghanistan kufanya utakavyo. Lakini hilo amelieleza katika hotuba yake mwezi March, wakati akiongeza wanajeshi zaidi mara ya kwanza. Hali haijabadilika, na ilionekana wazi katika udanganyifu uliotokea katika uchaguzi mkuu nchini Afghanistan.

Katika hotuba yake mbele ya wanajeshi wanaopata mafunzo katika chuo cha kijeshi cha West Point, ilionekana wazi, ni ugumu kiasi gani kwa mshindi huyu wa tuzo ya amani ya Nobel , kuweza kujitoa katika vita.

Mwandishi : Bergmann, Christina/ ZR / Kitojo Sekione

Mhariri:Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com