Misri yaahidi kutoufungua mpaka wa Rafah | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Misri yaahidi kutoufungua mpaka wa Rafah

Uamuzi umefikiwa leo hadi itakapojulikana hatma ya Gilad Schalit

default

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert aitaka Misri kusaidia kumkomboa Schalit

Misri imeahidi kuendelea kuufunga mpaka wake na ukanda wa Gaza kunakodhibitiwa na kundi la Hamas hadi pale mwanajeshi wa Israel anayeshikiliwa mateka atakapoachiliwa huru. Ahadi hiyo imetolewa kufuatia mazungumzo kati ya waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais Hosni Mubarak wa Misri huko Sharm el Sheikh hii leo. Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yamekuja ikiwa ni siku ya sita tangu kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Kundi la Hamas yaliyosimamiwa na Misri.

Ahadi hiyo imeangaliwa kama ni ishara kwa Israel kwamba Misri itajaribu kumkomboa haraka mwanajeshi wake Gilad Schalit anayeshikiliwa mateka tangu miaka miwili sasa na kundi lenye mafungamano na watawala wa Gaza yaani Hamas. Kwa mujibu wa msemaji wa waziri mkuu Olmert,Mark Regev mazungumzo ya saa mbili kati ya Olmert na Mubarak yamefikia makubaliano kwamba mpaka wa Rafah hautafunguliwa na shughuli hazitaendelea kama kawaida hadi pale atakapoachiliwa huru mateka huyo mwanajeshi wa Israel.

Wiki iliyopita Israel iliondoa baadhi ya vizuizi vyake katika eneo la Gaza kama sehemu ya mpango wa makubaliano ya kusitisha mapigano na wanamgambo wakipalestina lakini ilikataa kuruhusu mpaka wa Rafah ambao ni muhimu kwa watu wa Gaza ufunguliwe. Israel badala yake iliweka sharti kwamba ili mpaka huo ufunguliwe lazima paweko ubadilishanaji wa wafungwa.

Katika mkutano wa ana kwa ana hii leo kati ya Mubarak na Olmert wamezungumzia juu ya suala hilo la mateka wa Israel Gilad Schalit na hatua itakayofuata kuhusiana na makubaliano ya kusimamisha mapigano baada ya miezi ya umwagikaji wa damu.

Waziri mkuu Olmert amemuomba rais Hosni Mubarak kusimamia mazungumzo ya kina kama mpatanishi kwa lengo la kumkomboa mwanajeshi huyo wa Israel. Itakumbukwa kwamba Msiri imekuwa na jukumu kubwa muhimu kama msuluhishi katika kusimamia makubaliano ya kukomesha mapigano wakati Israel ikikataa kuonana moja kwa moja na kundi la Hamas ambalo inasema ni kundi la kigaidi,huku kundi la hamas nalo likikataa katakata kutambua haki ya kuwepo kwa taifa hilo la kiyahudi.

Makubaliano ya kusimamisha mapigano yalimsababishia waziri mkuu Olmert Kukosolewa sana nchini Isreal.Waisrael wanasema Olmert angepasa kuweka sharti la kuachiliwa huru mwanajeshi wake kabla ya kukubaliana na Hamas kusitisha mapigano. Mpaka sasa lakini makubaliano hayo ya amani yanaonekana kuzaa matunda kwani Israel imesimamisha opresheni zake za kijeshi katika Gaza na wanamgambo wa Gaza wamekomesha mashambulio ya roketi dhidi ya Israel. Hata hivyo makubaliano hayo hayahusiani na eneo la ukingo wa magharibi linalokaliwa na Israel ambayo inadai lazima iendelee na shughuli zake za kijeshi kuwalinda raia wake,hali ambayo wengi wanahofia itasababisha ghasia ambazo zitahujumu makubaliano hayo.

Misri imesema kuwa inaendelea na juhudi zake za kutafuta makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya pande hizo mbili. Kulingana na msemaji wa rais Mubarak wa Misri Suleiman Awad,waziri mkuu Olmert pamoja na waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak wameahidi kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yatazingatia pia kujitolea kwa Hamas katika hatua ya kufikia mazungumzo juu ya kuachiliwa huru Gilad Schalit na kuachiliwa mamia ya wafungwa wa kipalestina wanaozuiliwa kwenye jela za Israel.

 • Tarehe 24.06.2008
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQ6x
 • Tarehe 24.06.2008
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQ6x
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com