Merz: Vita Ukraine haviishi hadi Urusi idhoofike
13 Februari 2026
Akizungumza katika mkutano wa usalama unaofanyika mjini Munich Ujerumani, Merz amesema tayari dunia ipo katika nyakati hizo huku akisisitiza kwamba washirika wa Ukraine ni lazima wafanye kila wawezalo kuileta Urusi katika nafasi ambayo haitaona tena haja ya kuendelea na vita hivyo alivyoviita "vibaya kabisa."
Kansela huyo wa Ujerumani amesema bado juhudiza kuivunja nguvu Urusi hazijafika mahala zinapohitajika.
Ameongeza kuwa rais wa Urusi Vladimir Putinhajaonyesha nia ya kweli ya kujihusisha kikamilifu katika mazungumzo ya amani ya kusitisha uvamizi dhidi ya jirani yake Ukraine, uvamizi ambao umeendelea kwa miaka minne sasa.
Zelenskiy apokea droni mpya
Huku hayo yakiarifiwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepokea kwa mara ya kwanza droni mpya zilizotengenezwa kwa ushirikiano wa Ujerumani na taifa lake.
Zelensky amelitembelea eneo la siri, kunakotengenezwa droni hizo Kusini mwa Ujerumani.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius. amesema hatua iliyochukuliwa ni ya kuiunga mkono Ukraine kujilinda dhidi ya uvamizi na pia ni hatua inayonufaisha pia Ujerumani.
Kampuni mpya inayotengeneza droni hizo inayoitwa Quantum Frontline Industries, inalenga kupeleka droni angalau 10,000 kwa jeshi la Ukraine ifikapo mwishoni mwa mwaka huu 2026.
Kulingana na kampuni hiyo, imekuwa ikitoa droni kwa Ukraine tangu mwaka 2022.
Wakati sekta ya miundombinu Ukraine ikiendelea kushambuliwa na Urusi kuanza kuitegemea Ujerumani kwa upatikanaji wa silaha zake kutaongeza uzalishaji wake kupitia huko.
Droni zinazotengenezwa zinazojulikana kama Linza zinauwezo wa kubeba vitu vilivyo na uzito wa kilo mbili ikiwemo mabomu na makombora. Uzalishaji wake unatarajiwa kuongezwa zaidi mwaka ujao.
Merz amkosoa Orban
Wakati hayo yakijiri Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amejikuta akitupiwa lawama katika mkutano huo wa usalama kwa hatua yake aliyoichukua ya kuitembelea Urusi na kuonana na rais Putin.
Kansela Friedrich Merz ametumia lugha kali kumkosoa Orban kwa hatua hiyo lakini bila kumtaja jina.
Merz alisema " Kuna mtu ndani ya Umoja wa Ulaya aliyeitembelea Urusi mwenyewe, hakuwa na ruhusa ya EU na hakufanikiwa kwa chochote."
Mwezi Julai mwaka 2024, Viktor Orban alikwenda Moscow na kukutana na Putin ziara ambayo ilikosolewa na Umoja huo uliosema Orban anatishia kuudhoofisha umoja huo.
Lakini baadae kiongozi huyo wa Hungary alifanya ziara Ukraine na kukutana na rais Zelensky ambakoa alipendekeza usitishaji wa mapigano ili kuwezesha kufanyika majadiliano ya amani.