Merkel asema hatoshawishi chaguo la mrithi wake | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel asema hatoshawishi chaguo la mrithi wake

Kansela Angela Merkel amesisitiza kwamba hatoingilia mjadala kuhusu nani anayepaswa kuwa mgombea wa vyama ndugu vya siasa za wastani na mrengo wa kulia, mgombea ambaye atakuwa kiongozi mpya wa kundi hilo.

Kauli ya Merkel imekuja baada ya kiongozi wa jimbo la Bavaria, ambaye umaarufu wake umepanda katika kura za maoni wakati wa janga la virusi vya Corona kumkaribisha kwa hadhi kabisa katika jimbo hilo la  Bavaria.

Markus Soeder waziri mkuu wa Bavaria alimkaribisha Merkel alipotembelea kasri la Herrenchiemsee, jengo la kifakhari la karne ya 19 lililoko kwenye kisiwa kilichozungukwa na ziwa na lililojengwa baada ya kasri la kifahari la Ufaransa la Versailles.

Ziara hii ya Merkel imegubikwa na tetesi na ati ati nyingi kuhusu msukumano ulioko ndani ya vyama hivyo ndugu kuelekea suala la nani atakayegombea ukansela katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwaka 2021 msimu wa mapukutiko.

Angela Merkel anaiongoza Ujerumani tokea mwaka 2005 na ameshasema kwamba hatogombea muhula wa tano. Chama chake cha Christian Democratic Union, CDU, kinapanga kumchagua kiongozi mpya ambaye atakuwa ni kiongozi wa pili kwa chama hicho tangu Merkel alipojiweka pembeni mnamo mwaka 2018 mwezi Desemba

Deutschland | Coronavirus | Lockdown Gütersloh | Ministerpräsident Laschet

Waziri Mkuu wa jimbo la North-Rhine Westphalia Armin Laschet anawania pia uongozi wa chama cha CDU.

.

Kuna majina matatu ya wanaowania nafasi hiyo ya kuteuliwa kuwa mgombea atakayeshika bendera ya vyama hivyo kuwania Ukansela katika uchaguzi mkuu. Lakini janga la mripuko wa virusi vya Corona halijawasaidia wagombea wote hao.

Armin Laschet ambaye ni waziri mkuu wa Jimbo la North Rhine Westphalia alikuwa mpiga debe mkubwa wa kutaka hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo ziondolewe na amekosolewa kweli kweli kwa jinsi alivyoushughulikia mgogoro huu.

Wapinzani wake ni Friedrich Merz na Norbert Roettgen wote hawana majukumu ya kiserikali na wamekuwa na nafasi ndogo sana ya kuleta athari ya aina yoyote. Kwa maana hiyo macho yote yameelekezwa kwa Soeder ambaye ni kiongozi wa chama cha Bavaria cha Christian Social Union, CSU, ambacho ni chama ndugu na Christian Democratic Union cha Merkel. 

Soeder aongoza kura za maoni ya raia

Kura za karibuni za  maoni ya wapiga kura zimeonesha Soeder ambaye alikuwa ni kiongozi wa kwanza kufunga shughuli za kimaisha ndani ya jimbo lake mnamo mwezi Machi na amekuwa akisisitiza juu ya kuchukuliwa tahadhari katika kufungua tena shughuli, yuko katika nafasi ya juu akiwatangulia wengine.

Soeder lakini amekuwa akiyakwepa na kuyapuuza maswali kuhusu mustakabali wake kwa kusema kwamba nyumbani kwake ni Bavaria. Lakini pia amewafanya watu kuanza kumfuatilia baada ya hivi karibuni kusema kwamba mtu pekee anayeweza kujipambanua katika mgogoro huo ndiye anayeweza kugombea ukansela na pia kwa kitendo cha kumualika siku ya Jumanne Kansela Merkel katika mkutano wa serikali ya jimbo lake la Bavaria katika kasri la Herrenchiemsee.

Politischer Aschermittwoch - CDU Thüringen: Friedrich Merz

Fredrich Merz ni mgombea mwingine anaewania kuchukua uongozi wa chama cha CDU na yumkini kuwa kansela ajae wa Ujerumani.

Hakuna kansela yoyote aliyekuwa madarakani aliyewahi kushiriki mkutano kama huo. Kansela Merkel alipoulizwa ikiwa Soeder ana sifa za kuwa kansela, alijibu anajizuia kuzungumzia kuhusu mrithi wake na hatotoa kauli yoyote. Akaongeza kusema kwamba angefurahi sana kutembelea vikao vya mabaraza ya serikali za majimbo mengine.

Soma zaidi Annegret Kramp-Karrenbauer kutowania ukansela Ujerumani

Ni muhimu pia kutaja kwamba hakuna mgombea wa chama cha Christian Social Union, CSU, aliyewahi kuwa kiongozi wa Ujerumani, licha ya kwamba chama hicho kiliwahi kutoa mgombea katika miaka ya 1980 na 2002 lakini wote walishindwa kwenye uchaguzi mkuu na wagombea ukansela kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo wa shoto, Social Democratic, SPD.

Chanzo: Mashirika