Merkel amsisitizia Erdogan kuheshimu uhuru | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel amsisitizia Erdogan kuheshimu uhuru

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitiza umuhimu wa uhuru wa maoni katika mazungumzo na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipoizuru nchi hiyo kwa mara ya kwanza tangu kufanyika jaribio la mapinduzi.

Wakiwa katika mkutano wa pamoja mbele ya waandishi habari, Erdogan alisema yeye na Kansela Merkel wamezungumzia kuhusu yanayoendelea nchini Syria, Iraq na bahari ya Aegean.

Aidha Erdogan alisema aligusia pia suala la ushirikiano katika vita dhidi ya ugaidi, mgogoro wa wahamiaji pamoja na uwezekano wa kupiga hatua za pamoja katika vita vinavyoendelea nchini Syria.

Naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, alimsisitiza Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kuheshimu  maadili ya kidemokrasia ya uhuru wa kujieleza, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini humo tokea jaribio lamapinduzi ya kijeshi la mwezi Julai.

Merkel aliwaambia waandishi habari kwamba ameahidi kumuunga mkono Erdogan katika jitihada zake za kuwasaka waliohusika na uasi huo wa kijeshi. Hata hivyo Merkel amesisitiza kuwa uhuru wa kujieleza pamoja na tofauti za misimamo ya kisiasa yasivurugwe.

Türkei Ankunft Angela Merkel in Ankara (picture-alliance/Anadolu Agency/G. Balci)

Merkel wakati akiwasili mjini Ankara kwa ziara ya kiserikali tarehe 02.02.2017

Ujerumani imekuwa ikionyesha wasiwasi juu ya Uturuki na kusema kwamba inatumia hatua kali kuulenga upinzani wa kidemokrasia pamoja na wanahabari, na hilo linaweza kuuweka mashakani uhusiano wa nchi hizo mbili.

Merkel ataka waangalizi wa OSCE kura ya maoni

Kansela Merkel ameomba waangalizi kutoka Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE) watumwe nchini Uturuki kusimamia kura ya maoni ijayo, inayolenga kupanua mamlaka ya rais.

Upinzani nchini Uturuki umekuwa ukidai kuwa mageuzi yaliyopendekezwa yataharibu uwezo wa kisiasa wa kutathmini na kukosoa asasi nyengine za uongozi nchini humo, lakini Erdogan ameuelezea wasiwasi kuwa hauna msingi.

Kansela huyo wa Ujerumani ambaye anatarajiwa kukutana na wawakilishi wa vyama viwili vya kisiasa vya Uturuki amesema vyama vya upinzani ni sehemu ya demokrasia. Tangu lilipotokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi, Uturuki imekuwa ikikosolewa kwa kuwakandamiza wale wanaodai kuwa ni wafuasi wa waliopanga njama za jaribio hilo.

Türkei Treffen Angela Merkel & Recep Tayyip Erdogan (picture-alliance/Anadolu Agency/K. Azher)

Kansela Merkel akiwa katika mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara

Kuhusu kura ya maoni, Erdogan amesema anatarajia kupokea muswada wa mabadiliko ya kikatiba kutoka bungeni leo au kesho. Mara baada ya kuliidhinisha hilo, tume ya uchaguzi itatangaza rasmi tarehe ya kupigwa kura ya maoni, inayotarajiwa  mapema Aprili.

Erdogan  amesema mapendekezo hayo, ambayo yatapelekea mfumo wa bunge uliopo sasa kufutwa na badala yake kuwepo mfumo wa rais mwenye nguvu kubwa kabisa, hautokomesha mgawanyiko wa madaraka nchini humo. Erdogan amezidi kuyatetea mapendekezo hayo ya mabadiliko ya katiba kwa kusema yatarahisisha kazi katika tawi la utendaji, tofauti na malalamiko ya wakosoaji kwamba ni mabadiliko yatakayompa rais nguvu zaidi. Rais huyo wa Uturuki amesema mahakama itabaki kuwa na mamalaka yake kamili katika mfumo huo mpya wa uongozi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dpa/afp/

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com