1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MELBOURNE : Daktari wa India ashtakiwa

14 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBio

Polisi ya Australia imemfungulia mashtaka daktari wa India mwenye umri wa miaka 27 leo hii kutokana na uhusiano wake wa kizembe na wanaodaiwa kuhusika na njama za mashambulizi ya mabomu nchini Uingereza hapo tarehe 29 na 30 mwezi wa Juni.

Baada ya kushikiliwa kwa siku 12 Mohamed Hanneef amefikishwa kwenye mahkama ya Brisbane akishtakiwa kwa kutowa msaada kwa kundi la kigaidi.Amerudishwa tena rumande hadi hapo Jumatatu wakati ombi lake la kupatiwa dhamana litakaposikilizwa.

Mkuu wa jeshi la polisi nchini Australia Mick Keely amesema mashtaka hayo hasa yanahusu uzembe badala ya kuwa nia na kwamba mashtaka yanasema alikuwa mzembe kwa msaada fulani aliutowa kwa kundi hilo hususan kwa simu yake ya mkono kutumiwa na kundi hilo.

Iwapo atapatikana na hatia Haneef anaweza kufungwa kifungo cha miaka 15 gerezani.

Mke wa mtuhumiwa huyo Firdous aliyeko nchini India amesema madai hayo ni upuuzi na amemtaka waziri mkuu wa India aiingilie kati.

Wakati huo daktari wa tatu Sabeel Haneef amefunguliwa mashtaka nchini Uingereza kuhusiana na njama za kuripuwa mabomu London na Glasgow na anatarajiwa kufikishwa mahkamani hapo Jumatatu.