Mchango kwa Ukarabati wa Chernobyl | Masuala ya Jamii | DW | 19.04.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mchango kwa Ukarabati wa Chernobyl

Leo mkutano maalum umefunguliwa Kiev mji mkuu wa Ukraine, ukiwa na azma ya kuchanga fedha za kusaidia kukabiliana na madhara ya ajali ya mtambo wa nyuklia wa Chernobyl uliotokea miaka 25 iliyopita.

Ukrainian President Viktor Yanukovych, left, welcomes President of the European Commission Jose Manuel Barroso during their meeting in Kiev, Ukraine, Monday, April 18, 2011. (AP photo/Andriy Mosienko, Pool)

Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine (kushoto) na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso.

Umoja wa Ulaya pekee umeahidi kutoa Euro milioni 110 kusaidia kuugubika mtambo huo kwa kuta za zege. Rais wa Ukraine Viktor Yanukovych katika hotuba ya kuufungua mkutano huo mjini Kiev alisema kuwa Chernobyl ni maafa kwa dunia mzima kwa hivyo ulimwengu mzima unapaswa kushirikiana kupambana na janga hilo. Ajali ya kiwango kikubwa kama hicho haiwezi kuachiliwa Ukraine peke yake. Amesema ajali ya hivi karibuni nchini Japan pia imethibitisha kuwa matukio kama hayo ni changamoto kwa binadamu wote.

Kinu cha Chernobyl kilichomiminiwa zege hiyo miaka 25 iliyopita, sasa kina nyufa na matundu na hivyo mionzi ya sumu ya nyuklia inapenya. Ukarabati uliofanywa kati ya mwaka 2004 na 2008 umetumia vyuma kuimarisha baadhi ya kuta zilizogubika kinu hicho. Julia Marositsch anaefanya kazi katika kitengo cha ushirikiano wa kimataifa cha mtambo wa nyuklia wa Chernobyl anasema:

"Vyuma hivyo vitasaidia kuimarisha jengo hilo la zege kwa takriban miaka 15. Kwa hivyo kuna muda wa kufanya ukarabati na kumimina zege jipya ili kuwa na kuta imara zaidi."

This 1986 aerial view of the Chernobyl nuclear plant in Chernobyl, Ukraine shows damage from an explosion and fire in reactor four on April 26, 1986 that sent large amounts of radioactive material into the atmosphere. Ten years after the world's worst nuclear accident, the plant is still running due to a severe shortage of energy in Ukraine. (AP Photo/ Volodymyr Repik)

Mtambo wa nyuklia wa Chernobyl ulioripuka 26 Aprili, 1986

Kazi hiyo ya ukarabati inahitaji muda huo, kwani kazi ya mradi huo mkubwa ni ngumu kuliko vile ilivyotazamiwa kama anavyoeleza Heinz Smital, mtaalamu wa kinga ya mionzi ya nyuklia wa shirika la ulinzi wa mazingira Greenpeace.

"Haiwezekani kufanya kazi juu ya jengo hilo kwani katika sehemu hiyo viwango vya mionzi ya nyuklia ni vikubwa mno."

Gharama za ukarabati zinaongezeka kila mwaka. Kwa hivi sasa, inatathminiwa kuwa kutahitajiwa kiasi cha Euro bilioni 1 nukta 6 - na jumuiya ya kimataifa inatoa msaada - mfadhili mkubwa ni Umoja wa Ulaya. Na msaada huo unahitajiwa, kwani bado kuna hatari kubwa. Inatathminiwa kuwa asilimia 5 tu ya mionzi ya nyuklia ndio iliyotawanyika wakati wa mripuko. Hiyo humaanisha asilimia 95 bado zimo ndani ya mtambo huo. Na taka hizo za nyuklia lazima zizuiliwe ndani kwa njia yo yote ile anasema Heinz Smital wa Greenpeace.

Mwandishi:Nagel,Christina/ZPR/P.Martin

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com