Mbeki asifiwa kuwa muokozi wa Zimbabwe. | NRS-Import | DW | 25.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Mbeki asifiwa kuwa muokozi wa Zimbabwe.

Umoja wa Ulaya umeunga mkono kwa dhati jukumu ililonalo serikali ya Afrika kusini katika upatanishi wa mzozo nchini Zimbabwe.

default

Rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki akisalimiana na kiongozi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai baada ya kutiwa saini makubaliano ya kuanza majadiliano juu ya hali ya baadaye ya serikali nchini humo mjini Harare hivi karibuni.


Afrika ya kusini na umoja wa Ulaya wamemaliza mkutano wao wa kihistoria leo Ijumaa, wakati umoja huo ukiunga mkono kwa dhati jukumu la utawala huo wa Afrika kusini, kupatanisha katika mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe kuwa ni njia pekee ya kumaliza machafuko ya kisiasa nchini Zimbabwe.


Sekione Kitojo anaangalia mkutano huo uliofanyika mjini Bordeaux.


Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy , ambaye nchi yake inashikilia urais wa umoja wa Ulaya kwa sasa , amemmwagia sifa tele rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki kutokana na hatua yake ya kijasiri ya kuingilia mzozo wa Zimbabwe.

Tunaunga mkono kwa dhati upatanishi wa kijasiri unaofanywa na rais Thabo Mbeki na kuunga mkono wazo la kuumpa muda zaidi, Sarkozy amesema katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano wa kwanza baina ya umoja wa Ulaya na afrika kusini uliofanyika katika mji wa Bordeaux.

Sarkozy amesema kuwa juhudi za upatanishi za Mbeki zinapaswa kuungwa mkono, ana kuongeza kuwa hakuna njia nyingine inayowezekana hivi sasa na kila mtu katika bara la Ulaya anakubaliana na hilo.

Lakini Sarkozy amesema kuwa hatazungumza na rais Mugabe, kwasababu uamuzi wangu unatokana na yale aliyoyafanya ambayo ni mabaya.

Rais wa tume ya Ulaya Jose Manuel Barroso ameusifu mkutano huo kuwa ni wa kihistoria katika maendeleo ya ushirikiano, na kusema kuwa Afrika kusini ni mhusika kiongozi na anayeheshimiwa katika medani ya dunia. Mkutano huo uligubikwa na mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe pamoja na msimamo usiopinda wa Afrika kusini na umoja wa Ulaya kuhusu njia za kuutatua baada ya rais mkongwe Robert Mugabe kuchaguliwa tena katika uchaguzi ambao alikuwa mgombea pekee kufuatia duru ya kwanza iliyokuwa na utata.

Umoja wa Ulaya siku ya Jumanne ulipanua vikwazo vyake dhidi ya zimbabwe licha ya makubaliano yaliyofikiwa kupitia upatanishi wa rais Thabo Mbeki kati ya rais Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kuhusu mazungumzo juu ya kugawana madaraka.

Umoja wa Ulaya unamuona Mugabe kuwa ni mkandamizaji muonevu ambaye amekiuka haki za binadamu na kukandamiza demokrasia na kuuharibu uchumi wa Zimbabwe ambao hapo kabla ulikuwa ni mfano kwa mataifa ya Afrika na kuwa na ughali wa maisha kwa kiwango cha juu kabisa duniani.

Mbeki kwa upande mwingine , hadi sasa ameshindwa kumshutumu hadharani Mugabe, na anaonekana kupingana na jaribio lolote kumbinya kingozi huyo wa Zimbabwe na kusalim amri kwa mbinyo wa aina yoyote kutoka katika mataifa ya magharibi.

Siku ya Ijumaa , Mbeki alitaka kusisitiza kuwa upinzani dhidi ya Zimbabwe unapungua na kusema akijibu swali kuwa hajaomba kuondolewa kwa vikwazo. wote tunakubaliana kuwa ni muhimu kwa pande zote za kisiasa nchini Zimbabwe kusonga mbele kufikia makubaliano , juu ya kuunda serikali itakayojumuisha makundi yote pamoja na mpango wa pamoja utakaoielekeza Zimbabwe mbele.

Nafikiri kila mtu duniani analitaka hili kutokea haraka , amesema Mbeki. Nakubali kabisa moyoni msaada ulioelezwa na rais Sarkozy.

Upatanishi wa rais Mbeki uliodumu miezi 16 umeshutumiwa na wakosoaji kuwa yuko dhaifu mno mbele ya mzee Mugabe.

Mbeki amekwepa hata hivyo swali alipoulizwa iwapo anatafuta njia muafaka ya mzee Mugabe kujitoa uongozini, ambapo hadhi yake kama shujaa wa ukombozi bado kwa kiasi kikubwa haijafifia katika bara hilo.

Wazimbabwe itabidi kuchukua uamuzi juu ya nani anang'atuka lini, amesema Mbeki. Sio kitu ambacho kitatoka kutoka katika upatanishi amesisitiza.►◄
 • Tarehe 25.07.2008
 • Mwandishi Kitojo, Sekione
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ejp2
 • Tarehe 25.07.2008
 • Mwandishi Kitojo, Sekione
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ejp2
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com